Wachezaji 120 wateuliwa maandalizi ya Umisseta Wilaya ya Ilemela

Mwanza. Wachezaji 120 wamechaguliwa kuunda timu ya Wilaya ya Ilemela ambayo imeanza kambi jana Jumanne kujiandaa na Mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondanri nchini (Umisseta) ngazi ya Mkoa.

Mashindano ya Umiiseta Kitaifa yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 4 mwaka huu jijini Mwanza katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Bitimba.

Akizungumza jana wakati wa uteuzi wa kikosi hicho, Afisa Michezo wa Manispaa hiyo, Bahati Kizito alisema kuwa awali Wachezaji 400 walikuwa wakishiriki katika michezo ya soka, kikapu, mpira wa mikono, riadha, netiboli na sanaa.

Alisema kuwa wanaamini kikosi walichokiteua katika kila mchezo watafanya vyema na kuweza kupata idadi kubwa ya vijana watakaounda timu ya Mkoa wa Mwanza.

“Awali tulikuwa na wanamichezo 400 waliokuwa katika Kanda nne, ikiwa ni Bwiru, Busweru, Pasiansi na Bugogwa, ambapo tumechagua wachezaji 120 kutokana na mahitaji yetu,” alisema Kizito.

Aliongeza kuwa licha ya kuteua timu hiyo,bado wana changamoto mbalimbali haswa vifaa vya michezo kwa viongozi na wachezaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya NMB tawi la Rock City, Jacqueline Timoth alisema kuwa kutokana na taasisi yao kuwa wadau wa michezo nchini, watasaidia upatikanaji wa vifaa vya michezo.

“Kutokana na taasisi yetu kuwa mdau wa michezo nchini, tutatoa vifaa vya michezo mbalimbali ili kuisaidia timu hii kufanya vizuri kwenye mashindano hayo,” alisema Timoth.