WAMETISHA: Wafalme wa mataji Msimbazi

WAKATI nyota wengi wa Simba wakiwa na furaha ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu wameanza kushiriki Ligi Kuu Bara, ndani ya klabu hiyo kuna nyota saba ambao wana rekodi za maana.

Kama ulikuwa hufahamu nyota wakubwa wa Simba kama Said Ndemla, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shiza Kichuya na wengineo ndio wamefanikiwa kuvaa medali za ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza katika historia yao ya soka.

Kitendo cha Simba kukosa mataji ya Ligi Kuu kwa kipindi cha miaka mitano, kimewafanya nyota wake wengi kushuhudia medali zikivaliwa na wenzao kabla ya kufanikiwa kuzivaa kwa mara ya kwanza mwaka huu.

Sasa ndani ya ya timu hapakosekani wababe, humo ndani ya kikosi cha Simba unaambiwa kuna mastaa wenye medali za ubingwa kibao tu. Walizipataje? Soma makala haya kwa umakini.

Haruna Niyonzima (Mataji Matano)

Kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ndiye anayeongoza kutwaa mataji mengi ndani ya kikosi cha Simba, japo mengi alishinda wakati akicheza kwa watani zao, Yanga.

Niyonzima alianza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2012-2013, ikiwa ni mwaka wake wa pili ndani ya Yanga aliyojiunga nayo mwaka 2011. Niyonzima alitwaa taji hilo akiwa katika kiwango bora ambapo mara baada ya kumalizika kwa msimu, Mwanaspoti lilimpatia tuzo maalumu ya heshima kwa soka lake la ufundi.

Niyonzima alishinda mataji mengine ya Ligi Kuu akiwa na Yanga 2014/15, 2015/16 na 2016/17 kabla ya kutimkia Simba alikobeba taji msimu huu.

Emmanuel Okwi (Mataji Matatu)

Kinara wa mabao wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi, naye hajaachwa nyuma kwenye orodha ya nyota waliotwaa mataji mengi Msimbazi. Kwanza Okwi ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Simba waliokuwepo kwenye kikosi kilichotwaa taji la mwisho mwaka 2012 kisha kutwaa tena mwaka huu.

Ubingwa wa kwanza wa Okwi Msimbazi ulikuwa msimu wa 2009/10. Ubingwa huo ulinoga zaidi pale Simba ilipomaliza msimu bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Baada ya hapo Okwi alishinda taji jingine 2011/12 na baadaye kuondoka na kwenda kujiunga na timu ya Étoile du Sahel ambayo hakudumu nayo na kuamua kuondoka msimu huohuo wa 2013 na kujiunga na SC Villa nayo hakuweza kudumu nayo akaamua kurudi Tanzania na kujiunga na Yanga lakini hakuweza kumaliza msimu na klabu hiyo.

Msimu wa 2014-2015 alirudi katika klabu yake ya zamani Simba ambapo alicheza msimu mmoja na kuamua kuondoka na kwenda kujiunga na Sønderjyske ya Denmark.

Staa huyo wa Timu ya Taifa ya Uganda aliachana na wababe hao wa Denmark mwaka jana na kujiunga na SC Villa tena kabla ya kusajiliwa na Simba msimu huu ambao ameipa ubingwa mwingine.

Shomari Kapombe (Mataji mawili)

Beki bora zaidi wa kulia nchini, Shomary Kapombe naye yumo kwani mpaka sasa ameshinda mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo.

Kapombe alitwaa ubingwa wa kwanza msimu wa 2011/12 akiwa na Simba na baadaye mwaka uliofuata akaondoka na kujiunga na klabu ya AS Cannes iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Nne kule Ufaransa.

Baada ya kuachana na timu hiyo ya Ufaransa, Kapombe alirejea nchini na kujiunga na Azam FC ambayo aliichezea kwa miaka mitatu na kuambulia patupu kabla ya kujiunga tena na Simba iliyompa taji jingine msimu huu.

Mwinyi Kazimoto (Mataji Mawili)

Mkongwe huyo katika ligi naye ana medali kadhaa za kujivunia. Kazimoto ambaye aliamua kuachana na kazi ya Jeshi ili ajiunge na Simba mwaka 2011 naye amenufaika na timu hiyo kwani imempa mataji mawili ya heshima mpaka sasa.

Kiungo huyo alishinda taji lake la kwanza na Simba msimu wa 2011/12 kabla ya kutimkia Qatar alikojiunga na timu ya Al-Markhaiya aliyodumu nayo hadi 2015.

Msimu wa mwaka 2015-2016 alirejea Msimbazi kwa kishindo lakini amelazimika kusubiri mpaka msimu huu ili kuongeza taji jingine la Ligi Kuu.

John Bocco (Mataji Mawili)

Hebu sikia hii ya John Bocco. Straika huyo mwenye mabao 98 Ligi Kuu Bara, ameweka rekodi ya aina yake ya kutwaa ubingwa akiwa nahodha wa klabu mbili tofauti ndani ya Ligi Kuu.

Bocco alitwaa ubingwa wa kwanza akiwa nahodha wa Azam FC msimu wa mwaka 2013/14, japokuwa msimu huo haukuwa mzuri sana kwake kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Katika hali ya kushangaza, Azam iliachana na straika huyo mwishoni mwa msimu huu, hivyo kuamua kujiunga na Simba iliyompa heshima ya kuwa nahodha wa klabu hiyo, hivyo akaweka rekodi ya kutwaa mataji kama mchezaji kiongozi wa timu mbili tofauti.

WENGINE

Mbali na mastaa hao, pia kuna wengine walioshinda mataji mawili ni kipa Aishi Manula na kiraka Erasto Nyoni waliotwaa taji hilo wakiwa Azam 2013/14 na kisha kutwaa taji jingine wakiwa na Simba msimu huu. Mastaa hawa pamoja na Bocco, waliachana na Azam katika mazingira ya kutatanisha mwishoni mwa msimu uliopita.