Vigogo Yanga wateka straika

Muktasari:

  • Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 na juzi ikachapwa bao 1-0 mjini hapa, lakini habari njema ni kuhusu yule muuaji wa Yanga, Mtogo Arafat Djako ambaye ni straika tegemeo wa Wahabeshi hao.

YANGA imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Welaytta Dicha, lakini hesabu za mabosi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara ziko mbali kwelikweli.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 na juzi ikachapwa bao 1-0 mjini hapa, lakini habari njema ni kuhusu yule muuaji wa Yanga, Mtogo Arafat Djako ambaye ni straika tegemeo wa Wahabeshi hao.

Mpango mzima uko hivi. Mara baada ya mchezo huo wakati viongozi na wachezaji wa Welaytta Dicha wakiinamisha vichwa chini kwa huzuni, mabosi wa Yanga walikuwa pembeni ya straika huyo wakizungumza naye na ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Yanga.

Mwanaspoti ambalo lilikuwepo uwanjani hapo, lilishughudia mabosi hao wa Yanga ambao baadhi ni wajumbe wa Kamati ya Mashindano, wakichukua mawasiliano ya Arafat kisha kuendelea na harakati za kushangilia timu yao kusonga mbele. Straika huyo raia wa Togo ndiye aliyepachika bao pekee la Wahabeshi hao kabla ya kutiwa mfukoni na Abdallah Haji ‘Ninja’, ambaye alicheza soka la kupambana kinoma.

Bila kupoteza muda, fasta tu Mwanaspoti lilimfuata straika huyo na kupiga naye stori mbili tatu ambapo, alikiri kuzungumza na mabosi hao wa Yanga ambao pamoja na mambo mengine waliulizia mkataba wake.

Amesema kuwa, mkataba wake na Dicha unafikia tamati mwezi Juni, mwaka huu na yuko tayari kutua Yanga kama watafikia makubaliano kwani, soka ndio maisha yake.

“Ndiyo kama ulivyoona walikuja wale viongozi wa Yanga, tumezungumza kidogo na wameulizia mkataba wangu na kunipa pole na kunitaka nikuongeza jitihada uwanjani. Pia walitaka kufahamu kuhusu mkataba wangu ukoje, hapa unafikia mwisho Juni, mwaka huu.

“Kama watakuwa tayari basi hakuna tatizo tunaweza tukazungumza, niko tayari kuichezea Yanga kwani nimeona ni timu nzuri na ina mipango ya kutawala soka la Afrika,” alisema Arafat.

Hata hivyo, wakati mabosi hao wa Yanga wakiweka mambo sawa kwa Arafat, nahodha wao Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amegomea mpango huo akisema Yanga inahitaji straika hatari zaidi ya Mtogo huyo.

“Yule namba 10 (Djako) ni straika mzuri sana, lakini nadhani Yanga anahitajika mtu wa maana zaidi yake. Viongozi wanaweza kuweka mambo sawa, lakini akipatikana mwingine itakuwa bomba zaidi. Yule asiwe chaguo la kwanza,” alisema Cannavaro ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa Yanga katika kushauri wachezaji bora kusajiliwa.

Waethiopia waangusha sherehe

Katika hatua nyingine, licha ya Yanga kupokea kipigo cha bao 1-0 kwenye mchezo huo wa marudiano dhidi ya Dicha, mmiliki wa hoteli ya Rori ambako Yanga waliweka makazi amewafanyia sherehe ya kuwapongeza kwa kusonga mbele kwenye hatua ya makundi.

Tafrija hiyo fupi ilifanyika juzi usiku mara baada ya kikosi hicho kurejea hotelini hapo kutoka uwanjani, ambako baada ya chakula uongozi wa hoteli hiyo uliandaa keki maalumu na vinywaji kwa ajili ya wachezaji na viongozi.

Bosi wa hoteli hiyo Kidnemariam Asfawa, aliwaelezea Yanga kuwa ni timu ya pili kubwa kufikia hotelini hapo ikitanguliwa na Zamalek, lakini wamefurahishwa zaidi ya ujio wa Yanga kutokana na nidhamu nzuri ya wachezaji na viongozi.

Zamalek ilifikia hapo wakati ikija kuumana na Dicha na kukubali kipigo cha mabao 2-1 huku Yanga ikilala kwa bao 1-0 ingawa Yanga inajitofautisha kwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuitupa nje Dicha