Vigogo Yanga wakomaa na Manji

Muktasari:

Manji alitangaza kujiweka kando ndani ya klabu hiyo ambayo ameiongoza kwa mafanikio katika kipindi chote tangu alipoanza kuifadhili hadi kuwa Mwenyekiti wake huku akiipa mataji kibao na kuiwezesha kutamba anga za kimataifa.

KAMA kuna kitu ambacho Yanga hawataki kukisikia basi ni kuwaambia kuwa Yusuf Manji si kiongozi wa klabu hiyo.

Ndio! Yanga wamegoma kabisa kuachana na Manji na mpaka sasa wanaendelea kumtambua kuwa ndiye Mwenyekiti wa klabu hiyo yenye historia ya kibabe kwenye soka la Tanzania.

Manji alitangaza kujiweka kando ndani ya klabu hiyo ambayo ameiongoza kwa mafanikio katika kipindi chote tangu alipoanza kuifadhili hadi kuwa Mwenyekiti wake huku akiipa mataji kibao na kuiwezesha kutamba anga za kimataifa.

Iko hivi. Uongozi wa Yanga umeanza mchakato wa uchaguzi kwa ajili ya kujaza nafasi za viongozi ambazo zipo wazi, lakini nafasi ya Mwenyekiti ikiondolewa kwenye orodha ya nafasi zilizo wazi.

Hatua ya mabosi wa Yanga kuanza mchakato huo, imetokana na agizo la Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuwapa siku 75 mabingwa hao wa zamani ili kufanya uchaguzi ili kutimiza matakwa ya Katiba yao. Agizo hilo pia linaihusu Simba ambayo tayari imetangaza kuanza mchakato huo wa uchaguzi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Bakiri Makere, alisema nafasi ambazo zitawaniwa kwenye uchaguzi huo ni Makamu Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

“Mwenyekiti wa Yanga bado ataendelea kuwa Manji kwa sababu mpaka sasa hatujapokea barua inayoonyesha kwamba ameondoka katika nafasi hiyo hivyo, hatuna haja ya kufanya uchaguzi katika nafasi hii,” alisema.

Alisema wanalazimika kuanza rasmi mchakato ili kuwapata viongozi muhimu ambao, wataziba nafasi ambazo zipo wazi hadi sasa na kuongeza kuwa katika kikao walichoketi baadaye jana Jumatano ndio kitatoa taswira halisi na tarehe ya uchaguzi huo.

Wakati mchakato huo wa uchaguzi ukianza, kikosi cha Yanga kinaendelea kujifua mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya kuwachapa USM Alger kwenye mchezo wao ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ambayo inaendelea kujinoa chini ya kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera, inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili usiku.