Video: Hamisa Mobeto, Irene Uwoya waonja moto wa TCRA

Dar es Salaam. Mwanamitindo Hamisa Mobeto na mcheza filamu Irene Uwoya wameitwaa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwa makosa ya ukiukwaji wa maadili.

Waigizaji hawa walijikuta mbele ya kamati hiyo kwa kosa la ukiukwaji wa sheria ya maudhui mitandaoni wakikutwa na hatia ya kuweka picha zinazoonyesha utupu katika kurasa zao za Instagram.

 Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Varelia Msoka iliwataka wasanii hao kuomba radhi kwa ukiukwaji huo.

Uamuzi huo ulifikiwa na kamati baada ya wasanii hao kikiri kosa na kuahidi kutorudia tena waliyoyafanya.

Msoka alidai kuwa kamati iliridhishwa na utetezi na ushirikiano waliotoa wasanii hao baada ya kuitwa kujielezea kuhusu picha hizo.

Sanjari na hilo wasanii hao walikiri kosa na kuahidi kuwa mabalozi kwa wengine kuhusu sheria ya maudhui.

Kwa mujibu kamati hiyo Hamisa alifanya kosa la kuweka mtandaoni picha za ujauzito huku Irene kosa lake likiwa kuweka picha za nusu utupu akiwa ufukweni.

Kufuatia kosa hilo Hamisa amepwa onyo na kutakiwa kuomba radhi kwa kuweka tangazo kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza Hamisa aliomba radhi kwa watu wote waliokwazwa na picha hizo ana kuahidi kuwa balozi kwa wanamitindo wenzake wanaopiga picha kama hizo.

“Najua wengi hawana elimu tosha kuhusu hii sheria mpya ya mitandao ya kijamii na maudhui naahidi nitakuwa balozi mzuri ili wasije kuitwa huku kama ilivyotokea kwetu.”

Kwa upande wake Uwoya nae pia aliomba radhi na kuahidi kuwa hatorudia tena kuweka picha za aina hiyo mtandaoni.

Aidha aliiomba kamati ya maudhui kutoa semina kwa wasanii ili kuwapa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao.

“Naishukuru kamati iliniita na kuzungumza na mimi kama wazazi wangu sikutegemea ingekuwa hivyo na nitumie fursa hii kuomba radhi kwa wote ambao hawakupendezwa na picha yangu.”