VITA YA TATU YA DUNIA

Muktasari:

Ndicho anachosema kocha huyo wa Manchester City akiwaaambia mastaa wake wakielekea kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao Manchester United huko Old Trafford kesho Jumapili.

LONDON ENGLAND. PEP Guardiola amewaambia wachezaji wake: “Chonde chonde jamani msifanye faulo kizembe nje ya boksi, hawa jamaa watatumaliza.” Ndicho anachosema kocha huyo wa Manchester City akiwaaambia mastaa wake wakielekea kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao Manchester United huko Old Trafford kesho Jumapili.

Ndiyo kwanza Desemba, lakini mechi hiyo ya vigogo wa Manchester imebeba dhana halisi ya ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu. Wasiwasi wa Guardiola kwa wachezaji wake lipo kwenye vimo, kwamba Man United ina wachezaji wengi warefu, hivyo kuruhusu mipira ya adhabu au hata krosi zitawafanya kuwa kwenye wakati mgumu. Man City beki wake wa kati, Nicolas Otamendi kimo chake ni futi 5 na inchi 10, lakini anakwenda kukabana na straika Romelu Lukaku, mwenye urefu wa fiti 6 na inchi 3.

Unajua mechi hiyo ya Manchester derby ni kama Vita ya Tatu ya Dunia. Kila timu inataka kushinda. Guardiola anafahamu wazi, ushindi utamfanya aweke pengo la pointi 11 litakalomfanya kupumua kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo. Lakini, Jose Mourinho anafahamu wazi kwamba anahitaji kushinda kupunguza kasi ya Man City, huku akitaka kuendeleza rekodi yake nzuri ya kucheza mechi nyingi bila ya kupoteza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford. Straika wa Man City, Sergio Aguero kimo chake ni futi 5 na inchi 8, lakini anakwenda kukumbana na mabeki wa Man United, Chris Smalling, futi 6 na inchi 4, wakati Phil Jones ana futi 6 na inchi 1, huku Marcos Rojo akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 2. Hapa, Man City haiwezi kutoboa kwa mipira ya juu.

Fomesheni

Mourinho siku za karibuni kwenye mechi ngumu, ameonekana kutumia fomesheni ya 3-5-2, ambapo aliitumia kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Arsenal na aliitumia pia kwenye mechi dhidi ya Tottenham na Chelsea. Lakini, katika kuwakabili Man City, Mourinho anaweza kutumia fomesheni ya 4-2-3-1, ili kuwatumia mawinga Marcus Rashford na Anthony Martial kwa pamoja ili kupunguza kasi za kikosi hicho cha Guardiola kinachoshambulia kupitia pembeni.

Guardiola fomesheni yake ambayo amekuwa akiipendelea zaidi kwa msimu huu ni 4-1-4-1, ambapo wanapokuwa na mpira wananyumbulika na kuwa 4-3-3 inayowafanya kuwa na wachezaji wengi kwenye eneo la kushambulia, huku ile ya 4-1-4-1 ikiwafanya kuwa na uwezo wa kuanzia kukaba kwenye 18 ya goli la wapinzani.

Udhaifu wao

Acha Guardiola awe na wasiwasi kwa timu yake kutokana na mipira ya kutenga, amekuwa na udhaifu mkubwa. Katika michuano yote waliyoshiriki msimu huu, Man City imeruhusu wavu wake kuguswa mara 16, huku mara tatu ikiwa kwa mipira ya adhabu, wakati Man United wao kwenye mabao 15 iliyoruhusu, bao moja tu ndilo lililotokana na mipira ya adhabu.

Data zao

Man United hakika itakuwa kwenye mtihani mzito kwenye mchezo wao huo, kutokana na Man City kusheheni mafundi tu. Kwenye upande wa wakali waliopiga asisti nyingi kwenye ligi ya msimu huu, Man City ina wachezaji watatu katika tano bora, anaongoza Kevin De Bruyne mwenye asisti nane sawa na David Silva, huku Leroy Sane akiwa na asisti sita. Kwa upande wa Man United, anayeongoza kwa asisti ni Henrikh Mkhitaryan aliyepiga tano sawa na Paul Pogba, ambaye hatakuwamo kwenye mechi hii.

Mastaa wa Man City wanaofunika pia kwa pasi, ambapo Nicolas Otamendi amepiga pasi 1,256 na kufuatiwa na Fernandinho (1,252) kisha kuna David Silva (1,202) na De Bruyne (1,171) huku kwa upande wa Man United, Nemanja Matic akiachwa kwa mbali sana na pasi zake 1,008. Kwa maana hiyo, usishangae kuona Mourinho atakavyovurugwa kwa pasi za Guardiola katika mechi hiyo. Kitu ambacho Man United inatambia ni kipa wake, David De Gea kuokoa hatari nyingi, akifanya hivyo mara 53 kwa msimu huu. Kwa msimu huu, Man City imefunga mabao 46, wakati Man United imefunga mabao 35, huku kwa ujumla Man City imepiga pasi 10,972, wakati Man United imepiga pasi 7,379. Man United na Man City zinakwenda kwenye mechi hiyo, ambapo City wakiwa na rekodi ya kugusa mpira mara 13,704, wakati Man United imegusa mpira mara 10,363.

Rekodi zao

Kwa msimu huu, Man City haipoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England, ikishinda mara 14 kati ya 15 ilizocheza. Lakini, rekodi za jumla kwenye Ligi Kuu, Man United na Man City zimekutana mara 40, Man United imeshinda 20 na Man City 18, huku kukiwa na mechi nane zilizomaliza kwa sare. Kwenye mechi hizo, Man United imefunga mabao 59, wakati Man City imefunga mabao 51, huku kila timu ikipata penalti moja moja, Man United walifunga ya kwao, lakini Man City walikosa. Mechi hizo baina yao, Man United ilicheza mechi 15 bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa, wakati Man City imefanya hivyo mara nane tu. Man City imeshuhudia kadi moja tu nyekundu, wakati Man United katika mechi za Manchester derby kwenye Ligi Kuu England imeshuhudia kadi saba nyekundu. Mechi ya mwisho wa Old Trafford, wenyeji walichapwa 2-1, Man City ilifunga mabao yake kupitia kwa De Bryune na Kelechi Iheanacho, wakati lile moja la Man United lilifungwa na Zlatan Ibrahimovic.

Mechi nyingine

Liverpool na Everton wakati Arsenal itacheza na Southampton. Chelsea na West Ham, Burnley dhidi ya Watford huku Tottenham ikikwana na Stoke City.