VIDEO: Ubingwa Simba ni jasho,damu

IMEWACHUKUA miaka sita sawa na misimu mitano, Simba kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2017/18.

Miaka sita sio mchezo unaambiwa kwani, kama ni mtoto tayari ameanza chekechea na angesubiri mwakani kuanza darasa la kwanza, sio ajabu kwa miaka hiyo kukawepo ambaye ameshaanza elimu hiyo ya msingi.

Kabla ya msimu huu, Simba kuchukua ubingwa wao 19 mara yao ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2012, kipindi hicho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Dk Jakaya Kikwete.

Kuna matukio mengi yamepita katika kipindi hicho cha miaka sita ambayo, Simba ilikuwa ikiupigania ubingwa huo kwa jasho na damu.

SERENGETI BOYS YASHIRIKI AFCON

Mwaka jana, Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ walishiriki kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya Afcon kwa vijana wa umri huo kule Gabon.

Pamoja na kutovuka hatua ya makundi vijana hao waliiletea heshima Tanzania kwa kuwa miongoni mwa mataifa nane ambayo yalipata nafasi ya kushiriki.

SAMATTA ABEBA TUZO, UBINGWA

Wakati ukiwa mwaka wa pili kwa Simba bila ya ubingwa wa Ligi Kuu, mwaka 2015 nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alitwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Samatta akiwa TP Mazembe aliiongoza klabu hiyo kutoka DR Congo kuwafunga wababe wa Yanga, USM Alger kwa mabao 4-1 huku akifunga bao moja kwenye kila mchezo wa fainali.

Samatta alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani kwa mwaka huo ambao, alifunga mabao saba sawa na Bakri Al-Madina wa Al-Merreikh ya Sudan.

Tukio lingine ni kwa nahodha huyo wa Taifa Stars, kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji mwaka, 2016 na kusaini mkataba wa miaka minne na nusu.

MALINZI AWEKWA RUMANDE

Ndani ya mwaka wa sita bila ya ubingwa Simba, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza June 29, 2017, akikabiliwa na mashtaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha Dola za Marekani 375,418. 7

TFF YAPATA UONGOZI MPYA

Simba ikiendelea kusota kwenye mwaka wake wa tano, mchakato wa uchaguzi wa TFF ulikamilika Agosti 12 ili kusaka mrithi wa Jamal Malinzi.

Wallace Karia ndiye aliyeibuka mrithi wa Malinzi, ambaye bado kesi yake inaendelea na anasota rumande.

RUVU, LYON ZASHUKA NA KUPANDA

JKT Ruvu ambao wanafahamika kama JKT Tanzania na African Lyon, zilishuka daraja mwaka 2017 baada ya kumaliza msimu wa 2016/17 kwenye nafasi tatu za mwisho kwenye msimamo.

Timu hizo zimeonyesha ukomavu wa kupanda wa kurejea ndani ya mwaka huu kabla ya Simba kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

TAMBWE MFUNGAJI BORA YANGA

Baada ya kuachwa na Simba, straika Mrundi Amissi Tambwe alitua Yanga na kuwa mfungaji bora mwaka 2016 kwa kufunga mabao 21 kwenye msimu wa 2015/16.

Huo ulikuwa mwaka wa nne bila ya Simba kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku watani zao wa jadi Yanga, wakiendelea kutesa na kuwakejeli wenzao kwa kuwapa majina kibao kama wamatopeni, wahapahapa na mchangani.

TIMU ZA TANGA ZASHUKA

Wakati Tambwe akifanya yake kwenye mwaka huo wanne wa ukame wa mataji kwa Simba, tukio lingine kubwa ni kushuka daraja kwa timu zote tatu kutoka Tanga ambazo ni Mgambo, African Sports na Coastal Union.

AZAM YATWAA UBINGWA

Ndani ya mwaka wa pili kwa Simba bila ya ubingwa, Azam ilitangazwa kwa mara ya kwanza kuchukua ubingwa wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 62 na kuwaacha Yanga mdomo wazi ambao, walikuwa wakiwafuatia kwa ukaribu na pointi 56.

YANGA BINGWA MFULULIZO

Mtani wa Simba, Yanga ilionyeshwa umwamba kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kwenye miaka ya 2015,2016 na 2017. Miaka yote hiyo hali iliendelea kuwa mbaya kwa upande wao.

Ndani ya miaka hiyo, Yanga imetwaa ubingwa wa ligi mara nne huku pia wakifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili tofauti kwa mwaka 2016 na 2018 kabla ya Simba kutangaza ubingwa.

MSUVA AJIUNGA NA DIFAA

Tukio lingine ni aliyekuwa straika wa Yanga, Saimon Msuva kuanza maisha yake mapya katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco akitokea Jangwani mwishoni mwa mwaka jana.