VIDEO: Sisi ndo sisi

Muktasari:

  • Simba ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara msimu huu kabla ya mechi hiyo ya jana dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na iliyotumiwa kukabidhitaji la ubingwa baada ya kuutwaa mapema, lakini Kagera Sugar ikawatibulia furaha yao kwa kuwalaza bao 1-0.

MASHABIKI wa Simba jana walisahau kwa muda machungu ya kipigo ilichopewa timu yao mbele ya Rais John Magufuli na kujikuta wakishangilia kwa nguvu taji lao la Ligi Kuu Bara walilokabidhiwa na rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Simba ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara msimu huu kabla ya mechi hiyo ya jana dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na iliyotumiwa kukabidhitaji la ubingwa baada ya kuutwaa mapema, lakini Kagera Sugar ikawatibulia furaha yao kwa kuwalaza bao 1-0.

Bao la dakika 85 lililofungwa na straika Edward ‘Eddo’ Christopher kwa kichwa, liliinyima Simba furaha kwa muda kabla ya mashabiki kulipuka wakati wachezaji wao wakivishwa medali za ubingwa na kkabidhiwa kombe na Rais Magufuli.

“Tumebeba....Simba wafalme wenu...tumebeba...” waliimba mashabiki hao wa Simba waliofurika kwa wingi. Walisikika wakiimba hivyo pale nahodha John Bocco alipokabidhiwa taji.

Simba imenyakua taji hilo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011-2012 wakati ligi ikiwa bado haijamalizika likiwa la 19 kwao tangu Ligi Kuu Bara ilipoasisiwa mwaka 1965.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Simba kwa mara ya kwanza ilicheza saa 8 mchana kwenye jua kali na kujikuta ikipoteza yale makali yake huku mastraika wake wakipoteza nafasi nyingi za wazi za kuandikisha mabao mapema kipindi cha kwanza.

Dakika ya 19, beki wa kushoto wa Simba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alipiga krosi nzuri ambayo ilitua katika kichwa cha Shiza Kichuya ambaye alishindwa kumalizia vizuri.

Kiungo Said Ndemla dakika ya 22, naye alikunjua msuli kwa kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango la Kagera ambalo lilikuwa chini ya kipa mkongwe Juma Kaseja aliyekuwa nyota wa mchezo kwa kuinyima Simba mabao ikiwamo penalti ya dakika za nyongeza.

Kutokana hali ya joto kali, mwamuzi wa mchezo huo alitoa muda wa dakika moja kwa wachezaji kupoza makoo katika dakika ya 30 na kurudia tena katika kipindi cha pili.

Kagera iliyoweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu na kuvunja rekodi ya Msimbazi ya kucheza mechi 34 bila kupoteza, ikiwa ni sawa na siku 412 yaani mwaka mmoja na ushei, ilifanya mabadiliko dakika ya 31 kwa kumtoa Atupele Green na kumwingiza Omary Daga.

Dakika chache kabla ya mapumziko Okwi alimwekea pasi murua Shomary Kapombe, lakini shuti lake lilipaa nao Kagera ilijibu shambulio hilo kwa kiungo wake, Jafary Kibaya kupiga faulo iliyoonekana inaelekea wavuni kabla ya kipa, Said Mohammed ‘Nduda’ kupangua mpira uliokolewa na mabeki wa Simba waliongozwa na Paul Bukaba.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilikuwa imepata kona sita ambazo zote pia hazikuweza kuzaa matunda.

EDDO AWALIZA

Straika aliyekuzwa na Simba, Edward Christopher alitimiza ahadi yake ya kuwaliza Simba baada ya kufunga kwa kichwa bao la ushindi dakika ya 85 huku akimuacha Nduda akishindwa la kufanya.

Bao hilo lilipokewa kwa furaha na mashabiki wachache wa Yanga waliokuwa wakiishangilia Kagera Sugar, huku wale wa Simba wakionyesha kupigwa ganzi kwani hawakutarajia mambo yangewaendea vibaya mbele ya vijana hao wa Kagera.

Katika dakika tano za nyongeza Emmanuel Okwi akitafuta nafasi ya kufunga aliguswa na George Kavila na kujiangusha na mwamuzi kutoa penalti na akimpa kadi ya njano nahodha huyo wa Kagera, huku wachezaji wenzake wakimlalamikia mwamuzi.

Hata hivyo mkwaju wa Okwi aliyekuwa akisaka bao la 21 katika msimu huu, liliokolewa kiufundi na kipa Kaseja na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda, huku dakika zikiwa zinayoyoma.

Simba inapaswa kujiulaumu wenyewe kwa kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwa nafasi nyingi walizotengeneza, japo Kagera inayonolewa na Kocha

Mecky Mexime kuonekana ilikuja na dhamira ya kuwatibua Vijana wa Msimbazi.

RAIS AMWAGA PONGEZI

Mara baada ya mchezo huo, Rais Magufuli aliyekuwa na jukumu la kupokea mataji toka kwa timu ya taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys iliyotwaa katika michuano ya Vijana kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na ushindi wa pili wa Kombe la Dunia kwa timu ya taifa ya wasichana ya watoto waishio katika mazingira magumu waliotwaa Brazili.

Kabla ya kuzikabidhi timu hizo mataji na baadaye Simba, Rais alizimwagia sifa timu hizo na kutaka juhudi ziongezwe ili mwakani Tanzania ikiwa wenyeji wa Fainali za Afcon U17 2019 taji hilo la Afrika libaki nyumbani.

Simba: Nduda, Gyan, Tshabalala, Bukaba, Kotei/Mbonde/Bocco, Mkude, Nyoni, Kapombe, Okwi, Ndemla, Kichuya

Kagera: Kaseja, Magoma, Mguhi, Nyosso, Fakhi, Mwalyanzi, Makalai, Ramadhani/Kavila, Kibaya, Eddo, Atupele/Daga.