Penalti ya Kaseja yamchekesha JPM

Muktasari:

  • Lakini sasa, kipa huyo mkongwe aliyewahi kuzidakia Simba na Yanga, alikuwa mchezaji wa kwanza pia kumfanya Rais Magufuli acheke kwa furaha uwanjani hapo (Taifa) baada ya kupagua penalti ya Emmanuel Okwi ambayo ingeweza kuinusuru Simba na kipigo.

KAMA hujui ni kwamba Juma Kaseja ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza katika mchezo wa jana kati ya Simba na Kagera Sugar kuushika mkono wa Rais Dk. John Pombe Magufuli, wakati akikagua vikosi kabla ya mchezo.

Lakini sasa, kipa huyo mkongwe aliyewahi kuzidakia Simba na Yanga, alikuwa mchezaji wa kwanza pia kumfanya Rais Magufuli acheke kwa furaha uwanjani hapo (Taifa) baada ya kupagua penalti ya Emmanuel Okwi ambayo ingeweza kuinusuru Simba na kipigo.

Rais Magufuli alijikuta akicheka kwa furaha wakati kipa huyo wa Kagera akidaka penalti hiyo huku Wekundu wa Msimbazi hao wakiendelea kuweka rekodi ya kushindwa kupata ushindi mbele ya Rais wa nchi baada ya jana kulala bao 1-0 kwa Kagera na kutibua rekodi yao ya kuwa timu pekee iliyokuwa haijapoteza mchezo kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Iko hivi. Jana pale Uwanja wa Taifa, Simba ilikabidhiwa taji lake la ubingwa wa ligi msimu huu, lakini tukio lililomchekesha Magufuli kwa kufuraha kuliko muda mwingine wowote alipokuwa uwanjani hapo ni penalti ya Okwi kupanguliwa na Kaseja.

Katika mchezo huo Kagera ilitangulia kupata bao la kichwa la nyota wa zamani wa Simba, Edward Christopher, dakika ya 85 na katika muda wa nyongeza Simba ilipewa penalti baada ya Okwi kuonekana kuangushwa na George Kavila, japo marudio ya televisheni yalionyesha straika huyo alijirusha mbele ya mkongwe huyo.

Kabla ya penalti hiyo kila shabiki wa Simba alikuwa akishangilia akijua ndiyo nafasi pekee ya kulinda rekodi yao ya kutopoteza mchezo na Okwi anayeongoza kwa mabao alienda kupiga huku akijiamini.

Hata hivyo, Okwi alijikuta akiipoteza ilipodakwa kiufundi na kipa huyo wa Kagera na mara baada ya tukio hilo kamera za Mwanaspoti zilimnasa Magufuli akicheka kwa furaha sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Kipigo cha jana mbele ya Rais ni rekodi kwa Simba kwani katika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, Simba ililala mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kumtia simanzi Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi.

Kabla ya kuwakabidhi taji lao la 19, Rais Magufuli aliipongeza Simba kwa kufanikiwa ubingwa baada ya kusota kwa muda mrefu huku pia akilipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hasa uongozi mpya chini ya Rais Wallace Karia kwa kuanza vizuri.

Aidha Rais aliitaka Simba kujipanga vizuri ili we na uwezo wa kutamba kimataifa pia.