VIDEO: Mabondia Taifa walia hali magumu

Muktasari:

Katika mazoezi yao yanayoendelea kwenye uwanja wa ndani wa taifa, mabondia hao wameeleza changamoto nane zinazowakabili kuelekea kwenye michezo hiyo itakayoanza Aprili nchini Australia.

Dar es Salaam. Achana na ishu ya Mwanariadha Alphonce Simbu kuomba kujitoa timu ya taifa itakayaoshiriki michezo ya jumuiya ya madola, kule kwenye ngumi mabondia wanaojiandaa kuiwakilisha nchi kwenye michezo hiyo wameeleza namna wanavyojifua katika mazingira magumu kutokana na ukata.
Katika mazoezi yao yanayoendelea kwenye uwanja wa ndani wa taifa, mabondia hao wameeleza changamoto nane zinazowakabili kuelekea kwenye michezo hiyo itakayoanza Aprili nchini Australia.
"Tunafanya mazoezi katika mazingira magumu japo tunajiandaa kushiriki mashindano makubwa kama ya jumuiya ya madola," alisema nahodha wa timu hiyo, Haruna Swanga na kuendelea.
"Kwenye mazoezi yetu tunahitaji kuwa na daktari, tuwe na dawa, mabondia wapate japo maji ya kunywa na hata chai asubuhi, lakini vitu hivyo hakuna.
"Hatuko kambini, tunatumia nauli kila siku ya kuja mazoezi na kurudi nyumbani kutoka mfukoni na kuna wakati huna basi tungesaidia hilo tu japo kutuongezea hamasa na sisi tujione kama timu ya taifa.
"Tunachangamoto nyingine ya mapambano ya kujipima nguvu, tunahitaji tutoke tuzichape na mabondia wa nje ya Tanzania, lakini pia hata tuwekwe katika kambi ya kudumu, timu yetu ni nzuri sana, tatizo tunajifua katika mazingira magumu," alisema Swanga.
Kocha wa timu hiyo, Said Omary (Gogopoa) alisema timu hiyo inapaswa kuwa na muonekano wenye hadhi ya timu ya taifa, lakini  kwa sasa kitu hicho hakipo.
"Timu ilipaswa kufanya mazoezi ikiwa na sare inayoitambulisha kama timu ya taifa, lakini kutokana na aina ya mchezo mabondia walipaswa japo kupata chai asubuhi hata maji ya kunywa ni shida.
Aidha, mabondia hao waliiomba Serikali, Taasisi na wadau wa michezo nchini kujitokeza kuwasapoti huku nao wakiahidi kufanya vizuri kwenye michezo ya madola ambayo msimu huu Tanzania itawakilishwa na timu tano.
Michezo mingine ni mpira wa meza, kuogelea, paralimpiki na riadha ambayo tayari nyota wa mchezo huo, Alphonce Simbu ameomba kujitoa kwenye timu ya taifa ili akashiriki mbio za London marathoni ambazo bingwa anaondoka na mamilioni ya fedha.