VIDEO: Gor Mahia kuwakosa nyota watano wakiivaa Yanga SC

Muktasari:

Kwa mujibu wa kikosi cha Kogalo kilichowekwa bayana na Kocha Dylan Kerr ni kwamba, Kipa namba moja Boniface Oluoch, Beki kisiki asiye na masihara, Joash Onyango 'The Bull', Straika mpya Mustafa Francis, kiungo Mshambuliaji George Odhiambo 'Blackberry' na Kiungo Ernest Wendo, wote watakosa mtanange huo.

Nairobi, Kenya. Mabingwa wa soka nchini, Gor Mahia, wanashuka dimbani leo, Jumatano kuwavaa Yanga SC ya Tanzania, katika mchezo wa tatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa ugani Kasarani, Nairobi, bila nyota wake watano, Mwanaspoti Digital imefahamu.


Kwa mujibu wa kikosi cha Kogalo kilichowekwa bayana na Kocha Dylan Kerr ni kwamba, Kipa namba moja Boniface Oluoch, Beki kisiki asiye na masihara, Joash Onyango 'The Bull', Straika mpya Mustafa Francis, kiungo Mshambuliaji George Odhiambo 'Blackberry' na Kiungo Ernest Wendo, wote watakosa mtanange huo.


Onyango atakosa mechi hii akitumikia adhabu baada ya kulimwa kadi nyingi za njano, Oluoch anauguza jeraha, Straika Mustafa (Sajili mpya), atakosa kutokana na sababu binafsi huku Wendo na Blackberry wakiuguza majeraha.


Akizungumza na wanahabari, Kocha mkuu wa mabingwa hao mara 16 wa Ligi Kuu ya soka nchini, Muingereza Dylan Kerr, alisema kukosekana kwa mastaa hao sio tatizo kwani kikosi chake kiko fiti kalikiti kuwavaa Yanga, ambao alisema anawajua vizuri tu.


“Joash (Onyango) amefungiwa.  Boniface (Oluoch) ni majeruhi na Mustafa (Francis) ana sababu binafsi ambazo nisingependa kuyazungumzia hapa. Kikosini nina watu wengi, tuko tayari kwa mchezo na hakuna haja ya kuwa na hofu. Yanga ninawafahamu kwa hiyo msiwe na wasiwasi, tunashinda," alisema Kerr


Gor Mahia, ambao wanaongoza msimamo wa ligi kuu Kenya, wanaingia katika mchezo huu wakiwa hawajaandikisha ushindi hata mmoja hivyo ni lazima kuifunga Yanga ambayo nayo ina hali kama ya Kogalo kwani na wao hawajashinda.


Mara ya mwisho mabingwa hawa walikutana Julai 18, mwaka 2015, kwenye uwanja wa taifa Jijini Dar es Salaam, katika michuano ya Kombe la Kagame ambapo Kogalo waliibuka wababe kwa ushindi wa 2-1.