VAR yatua Ligi Kuu England kukata fitna

Muktasari:

  • Mechi 15 za wikiendi ijayo katika Ligi Kuu ya England zitaangaliwa katika VAR mara ligi hiyo itakapowadia wikiendi ijayo lakini hata hivyo, maamuzi ya ndani ya uwanja hayataathiriwa na mfumo huo moja kwa moja.

FITINA inakaribia kumalizika pale England. Baada ya utata mwingi wa maamuzi katika Ligi Kuu ya England hatimaye waamuzi wataanza rasmi mazoezi ya kuangalia marudio ya maamuzi kupitia video katika mfumo wa VAR.

Mechi 15 za wikiendi ijayo katika Ligi Kuu ya England zitaangaliwa katika VAR mara ligi hiyo itakapowadia wikiendi ijayo lakini hata hivyo, maamuzi ya ndani ya uwanja hayataathiriwa na mfumo huo moja kwa moja.

Ligi Kuu ya England imeamua kutotumia mfumo wa VAR katika msimu huu licha ya mafanikio ya mfumo huo katika Kombe la Dunia kule Russia, lakini endapo majaribio hayo yatakuwa na mafanikio kuna uwezekano msimu ujao mfumo huo ukaanza kutumika England.

Mechi tano za siku ya Jumamosi ambzo zitachezwa saa 11 jioni zitaangaliwa katika mfumo huo kutoka katika ofisi ya waamuzi wa England, Stockley Park lakini waamuzi wataruhusiwa kuendelea na maamuzi yao bila ya kuingiliwa ikiwa ni sehemu ya mazoezi tu.

Baadhi ya mechi ambazo zitatazamwa kwa mfumo huo ni kuhesabu makosa au usahihi wa wachezaji ni pamoja na pambano kati ya Newcastle na Arsenal litakalochezwa St James Park. Jingine ni pambano kati ya Chelsea na Cardiff katika Uwanja wa Stamford Bridge pamoja na lile la Manchester City dhidi ya Fulham Etihad.

Waingereza bado wanasita kuutumia mfumo huo lakini tayari mfumo huo umekuwa ukitumika katika Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga pamoja na Ligi Kuu ya Italia Serie A tangu msimu uliopita wakati Hispania wameanza kutumia mfumo huu msimu huu.

Katika soka la Kiingereza mfumo huo ulitumika kwa mara ya kwanza katika Michuano ya Kombe la Ligi maarufu kama Carabao lakini imekuwa haitumiki katika ligi pamoja na michuano mingine maarufu ya FA.

Majaribio hayo pia yana lengo la kujua kama maafisa wanaweza kutumia mfumo huo katika mechi nyingi kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa katika Kombe la Dunia ambapo timu chache zilikuwa zinacheza kwa wakati mmoja.

Katika Kombe la Dunia kule Russia VAR ilitumika kwa mara ya kwanza katika pambano la fainali Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Croatia jijini Moscow ambapo Ufaransa ilipewa penalti katika dakika ya 38 ya ambayo ilifungwa na staa, Antoine Griezmann.

Katika tukio hilo, mwamuzi wa kimataifa wa kutoka Argentina, Nestor Pitana alitonywa kuhusu uwezekano wa staa wa Croatia, Ivan Perisic kuunawa mpira wakati akijaribu kuokoa mpira wa adhabu wa Ufaransa. Ufaransa iliongoza 2-1.

Kabla ya hapo, tayari mfumo huo ulikuwa umetumika mara nyingi ingawa ulileta utata katika pambano kati ya Nigeria na Argentina wakati mwamuzi alipokwenda kuangalia marudio ya kunawa kwa mpira na beki mmoja wa Argentina lakini bado hakuipa penalti Nigeria.

Mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Fifa ilitangaza mfumo huo ulikuwa na mafanikio makubwa na utaendelea kutumika katika michuano mbalimbali iliyo chini yao.