Uzunguni wapiga hesabu kusajili mastaa wapya

Muktasari:

  • Kocha wa mabingwa hao Shabani Isango ‘Teacher Ndevu’ alisema kuwa kujizatiti kwa wachezaji wake ndio sababu imewafanya kufikia malengo na sasa wanaanza maandalizi ya RCL.

Kilimanjaro. Ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa wa Kilimanjaro  imemalizika mwishoni mwa wiki kwa timu ya Uzunguni Fc kutwaa ubingwa baada ya kuifunga timu ya Forest kwa mikwaju ya penati 5-4 mchezo uliopigwa uwanja wa Mwalimu Nyerere Complex.

Timu ya Uzunguni ilikuwa ya kwanza kuzifumania nyavu za wapinzani wao baada ya Mario Swai kuiandikia bado timu hiyo dakika ya tisa lililowaweka kifua mbele hadi mapumziko.

Kipindi cha pili timu ya Forest iliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Kulwa Hassan dakika ya 54  kabla ya Ibrahim Shabaan wa Uzunguni kupaisha mkwaju wa penati dakika ya 65 na kufanya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1 na kupelekea zikienda dakika 120 ambazo hazikuzaa matunda kwa timu zote.

Katika hatua ya mikwaju ya penati Abdallah Kombo wa Uzunguni alikosa mkwaju wake kabla ya Mario Swai na Mwita Matiku nao kupaisha mikwaju yao ya penati na kuiwezesha Uzunguni kuwa mabingwa kwa penati 5-4.

Hata hivyo kocha mkuu wa timu ya Forest Erick Sanga alisema kuwa kujiamini kupita kiasi kwa wachezaji wake ndio sababu iliyowafanya kushindwa kupata ushindi katika mchezo huo.

“Tumegundua wenzetu wakichezesha wachezaji wawili kinyume na kanuni za soka na tayari tumewasilisha malalamiko yetu kwa uongozi wa kamati ya ligi ili kuona haki inatendeka maana haiwezekani wachezaji wacheze ligi mbili kwa wakati mmoja,” alisema Sanga.

Kocha wa mabingwa hao Shabani Isango “teacher ndevu” alisema kuwa kujidhatiti kwa wachezaji wake ndio sababu imewafanya kufikia malengo na sasa wanaanza maandalizi ya RCL.

“Tayari nimewaona wachezaji 15 ambao watatusaidia kwenye maandalizi ya ligi ya mabingwa wa Mikoa (RCL) endapo uongozi utakubali kuwasajili ili kupata timu yenye ushindani,” alisema Isango.

Timu ya Forest inapoteza mara ya pili kuutwaa ubingwa wa mkoa wa Kilimanjaro baada ya msimu uliopita kutinga hatua ya fainali na kuondolewa na timu ya New Generation.