Uwanja wa Ndani Taifa mambo freshi!

Muktasari:

  • Dk Mwakyembe asema ataufanyia marekebesho uwanja huo wa ndani ambao umekuwa ukitumiwa kwenye michezo mbalimbali ya mpira wa kikapu na mpira wa wavu kabla ya mashindano yajayo ya Klabu Bingwa Kanda ya Tano.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameahidi kuufanyia marekebisho makubwa Uwanja wa Ndani Taifa ili kuwa na kiwango cha kimataifa.
Ahadi hiyo, Mwakyembe aliitoa kwenye zoezi la ugawaji zawadi za mashindano ya Kanda Tano ‘FIBA Zone V’ kwa vijana wenye  umri chini ya miaka 18   ambayo yalimalizika juzi kwa timu za Tanzania kuwa washindi wa tatu.
Dk Mwakyembe alisema ataufanyia marekebesho uwanja huo wa ndani ambao umekuwa ukitumiwa kwenye michezo mbalimbali ya mpira wa kikapu na mpira wa wavu kabla ya mashindano yajayo ya Klabu Bingwa Kanda ya Tano.
“Nawashukuru wadau wote ambao mmefanikisha kufanyika kwa mashindano haya na nitoe pongezi kwa washiriki wote na hongera kwa timu zilizofanya vizuri,” alisema Waziri huyo.
Timu ya Tanzania kwa wanaume imeshika nafasi tatu baada ya kuifunga Sudan kwa pointi 48-41 katika mchezo wa mshindi wa tatu. Rwanda iliibuka kuwa  bingwa wa mashindano hayo kwa kuifunga Uganda.
Upande wa wanawake nao, Tanzania imemaliza kwenye nafasi ya tatu, licha ya kufungwa  michezo yote na wapinzani wao, Uganda na Rwanda ambao walionekana kuwazidi uwezo.
Kumaliza kwenye nafasi hiyo kumetokana na uchache wa timu ambazo zimeshiriki katika mashindano hayo ambazo ni tatu, bingwa  Rwanda na mshindi wa pili, Uganda.
Mashindano ya Klabu Bingwa kanda ya tano ‘FIBA Zone V Club Championship’ yanatarajiwa kufanyika nchini Septemba 30 hadi Oktoba 7 mwaka huu.