Real, Barca, Man United kibaruani Ulaya

Muktasari:

Real Madrid inashikiria rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa mara 11 na sasa ni bingwa mtetezi

NYON, USWISI.MCHAKAMCHAKA wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unaendelea wiki huu ambapo vigogo Real Madrid, Barcelona na Manchester United watahakikisha wanapanga vikosi vya maana ili kupata tiketi yao ya kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora.

Liverpool, Chelsea na Juventus nazo hazipo kwenye nafasi ngumu ya kupenya, lakini mashaka makubwa yapo Atletico Madrid, ambao wanaweza kuaga mapema tu michuano hiyo sawa na ilivyo kwa wakali wa Serie A msimu huu, Napoli.

Real Madrid inayoonekana kuwa kwenye ubora duni msimu huu, watahitaji kushinda ugenini kwa APOEL kujihakikishia nafasi, wakati wenzao kwenye kundi lao, vinara Tottenham Hotspur watakuwa na shughuli huko Ujerumani kuwavaa Borussia Dortmund.

Mechi hizo zote zinapigwa leo Jumanne, sambamba na Napoli watakaokuwa nyumbani kuwakaribisha Shakhtar Donetsk, Monaco watakipiga na RB Leipzig, Sevilla na Liverpool, Spartak Moscow na Maribor, Besiktas na Porto na Manchester City wao watakuwa Etihad kuwakaribisha Feyenoord.

Kesho, Jumatano, michuano hiyo itaendelea kwa Man United wakiwa ugenini kwa FC Basel huku huko Turin kukiwa na bonge la mechi kati ya Juventus na Barcelona.

Bayern Munich wakisafiri kuifuata Andetletch, PSG watakuwa nyumbani kuwakaribisha Celtic na Atletico Madrid watakipiga na AS Roma, huku Sporting CP watakuwa mwenyeji wa Olympiakos, Chelsea wakiwa ugenini kwa Qabarag na CSKA Moscow watakuwa kwao kucheza na Wareno Benfica.