Simba, Yanga kufunga mwaka

Muktasari:

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema mechi 16 kati ya 152 zitacheza kuanzia saa 8:00 mchana.

Dar es Salaam. Huondo wa Ligi Kuu Bara utarejea Desemba 29 baada ya kusimama kwa wiki mbili kupisha mashindano yaKombe la Chalenji yanayoendelea nchini Kenya.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema mechi 16 kati ya 152 zitacheza kuanzia saa 8:00 mchana. 

"Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8 kamili mchana, hadi saa 4 kamili usiku," alisema Alfred.

Alisema uamuzi huo umefanywa ili kuongeza idadi ya mechi ambazo zinataonyeshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi.

Desemba 29 kutakuwa na mchezo mmoja pekee kati ya Azam  dhidi ya Stand United  utakofanyika kuanzia saa 1:00 usiku, wakati Desemba 30 Ndanda itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara,Lipuli itacheza na Prisons wakati Mtibwa Sugar itaikabili Majimaji .

Michezo ya Desemba 31 ni kati ya Mbao dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza,Njombe Mji itacheza na Singida United wakati  Januari Mosi Mbeya City itaikabili Kagera Sugar na Mwadui kucheza na Ruvu Shooting.

Alisema baada ya raundi ya 12 Ligi Kuu itasimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.