Usisahau mastaa hawa waliwahi kucheza timu moja

KUNA baadhi ya mastaa ambao hauwezi kuamini kwamba waliwahi kucheza timu moja katika siku za nyuma. Kila ukijaribu kuunganisha matukio unapata wakati mgumu kuamini kuwa waliwahi kucheza timu moja wakati fulani

Dele Alli na Alan Smith - MK Dons

Mpaka sasa Alli ana umri wa miaka 21 tu na anatamba katika Ligi Kuu ya England. hauwezi kuamini kwamba kila unapowaza kuhusu maisha ya staa wa zamani wa Leeds United na Manchester United, Alan Smith unakosa kujua ni namna gani mkongwe huyu mwenye umri wa miaka 37 sasa alicheza na Alli mahala. Ni kweli, walikutana katika klabu ya MK Dons ya daraja la kwanza. Wakati Alli alianza kuchanua na maisha yake ya soka, Smith alikuwa anaelekea mwisho katika maisha ya soka.

Aguero na David De Gea - Atletico Madrid

Timu mbili za Manchester ziliyaachanisha maisha yao ya soka. Kila mmoja kwa sasa ni mchezaji muhimu na anayeheshimika sana katika timu yake lakini usishangae kuona Aguero na De Gea wakipiga stori mara baada ya kumalizika kwa pambano la watani wa jadi wa jiji la Manchester. Wawili hawa waliwahi kukipiga pamoja katika klabu ya Atletico Madrid kabla ya Aguero kwenda Man City na De Gea kwenda Man United.

Marouane Chamakh na Mauricio Pochettino - Bordeaux

Unaweza usiamini hili kwa sababu kwa sasa mmoja ni mshambuliaji ambaye anamaliza siku zake za kucheza soka la juu, wakati mwingine ni kocha mkali anayekuja juu katika klabu ya Tottenham Hotspurs. Wanaonekana kuwa watu wawili tofautu lakini ukweli ni kwamba wawili hawa waliwahi kucheza pamoja katika klabu ya Bordeaux ya Ufaransa. Baadaye Pochettino alikwenda klabu ya Espanyol alikomalizia maisha soka, wakati Chamakh alikwenda Arsenal kwa uhamisho huru.

Ramsey na Hasselbaink - Cardiff City

Kwa haraka haraka akili yako inakutuma kwamba Hasselbaink alicheza wapi? Ni wazi kwamba utawaza zaidi Leeds United na Chelsea. Ramsey? Yupo Arsenal. Hata hivyo wawili hawa waliwahi kukutana katika klabu ya zamani ya Ramsey Cardiff City. Wakati Hasseibaink alikwenda huko kumalizia maisha yake ya soka, Ramsey alikuwa anaanza kuwika kiasi cha kuwindwa na klabu kubwa kabla ya kutua Arsenal. Walicheza pamoja mwaka 2007.

Dimitri Payet and Joe Cole - Lille

Wote wamewahi kucheza West Ham kwa nyakati tofauti. Lakini hii haimaanishi kwamba wawili hawa hawajawahi kucheza katika timu moja. Ukweli ni kwamba wote walikutana katika klabu ya Lille ya Ufaransa wakati Cole alipoamua kufunga safari yake ya nje ya nchi tofauti na wachezaji wengi wa Kiingereza. Dunia ni ndogo.

David Beckham and David Moyes - Preston

Moja kati ya wachezaji wawili ambao hauwezi kuamini kwamba walicheza timu moja. Hasa pale unapofikiria jinsi ambavyo David Beckham alikuwa jina kubwa katika soka wakati wajina wake David Moyes umemsikia zaidi katika suala la ukocha. Hata hivyo wawili hawa waliwahi kucheza soka pamoja wakati Moyes akiwa mwanasoka. Ilikuwa ni katika kipindi ambacho kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alimpeleka Beckham kwa mkopo klabu ya Preston ili kupata uzoefu na huko alikutana na Moyes.

Ivan Rakitic and Mesut Ozil - Schalke

Leo Rakitic ni kiungo muhimu katika kikosi cha Barcelona wakati Ozil ni kiungo muhimu katika kikosi cha kocha, Arsene Wenger pale Arsenal. Kabla ya hapo, Ozil alikuwa akikipiga Real Madrid lakini tayari alishakutana katika kikosi kimoja na Rakitic katika soka la Ujerumani wakati wote walipokuwa wanakipiga katika klabu ya Schalke kabla ya kila mmoja kufuata mpango wake.

Adebayor na Patrice Evra - Monaco

Marafiki wenye tabia zinazofanana. Wote wamecheza sana soka la Kiingereza akini hauwezi kujua kwamba zamani waliwahi kuwa na muunganiko katika klabu moja ya Ufaransa. Wakati huo wakiwa bado wabichi waliwahi kukutana katika klabu ya Monaco ya Ufaransa kabla ya Arsenal na Manchester United kuzinasa saini zao.

Jordi Alba na Isco - Valencia

Kwa sasa wanacheza katika timu hasimu za Hispania Barcelona na Real Madrid. Usishangae sana kuona siku moja Alba na Isco wakibadilishana jezi kwa sababu wamefahamiana zamani na hawakujuana barabarani. Waliwahi kukipiga kwa pamoja katika klabu ya Valencia kabla ya kudakwa na klabu kubwa siku za usoni.

Juan Mata and David Silva - Valencia

Kama ilivyo kwa Isco na Alba, mastaa hawa wawili wa Hispania nao waliwahi kucheza pamoja katika klabu hii ya Valencia. Ni klabu za jiji la England tu ndizo ambazo ziliwatenganisha. Wakati Mata alikwenda Chelsea, Silva alikwenda Manchester City. Kwa sasa wameendelea kutenganishwa kihasimu zaidi baada ya Mata kujiunga na Man United.