Usimchukulie poa Chifu wa Kauzu FC

Muktasari:

  • Chief alianza kujulikana rasmi na wadau wa soka nchini, mwaka 2014 kupitia Kauzu FC kwa kuongoza kundi la mashabiki wenzake kuishangilia timu hiyo, lakini yeye alikuwa na kitu cha kipekee kilichofanya aonekane wa kipekee dhidi ya wengine.

BINADAMU yeyote chini ya jua ana njia zake za kufanikiwa na kufikia malengo ya maisha yake ambavyo anataka yawe. Basi ndivyo ilivyo kwa shabiki maarufu wa Kauzu FC, Juma Ally ‘Chief’, jamaa ana stori ya kusisimua na kuchekesha iliyomfanya ajulikane ndani na nje ya Bongo.

Chief alianza kujulikana rasmi na wadau wa soka nchini, mwaka 2014 kupitia Kauzu FC kwa kuongoza kundi la mashabiki wenzake kuishangilia timu hiyo, lakini yeye alikuwa na kitu cha kipekee kilichofanya aonekane wa kipekee dhidi ya wengine.

Maajabu ya kubebwa ndani ya ungo yalifanya awe gumzo katika michuano hiyo, huku wengine wakidhania pengine ni mchawi, kutokana na mkononi mwake kubeba kibuyu na usinga ambavyo kwa tafsiri za Kiswahili tulivyolelewa zinaonekana kama imani za kishirikina.

Chief hakuishia kubebwa kwenye ungo, aliendelea kufanya vituko vya hapa na pale vilivyofanya Ndondo Cup iwe na mvuto wa hali ya juu, huku wengi wakiwa wanahitaji kumuona anafananaje, lakini pia, mashabiki wa timu nyingine wakiiga ubunifu na staili zake, hata hivyo hawakuweza kumfikia.

Mwanaspoti likaona isiwe tabu, likafunga safari mpaka nyumbani kwake Chamazi nje ya Jiji la Dar es Salaam ili kujua uhalisia wa maisha yake na kufanya naye mahojiano ya kina na akafunguka mengi tofauti na vile anavyojulikana akiwa katika kazi ya soka.

FAMILIA

Jamaa ni msela fulani hivi, ukimtazama kwa haraka haraka unaweza ukamchukulia mhuni wa mtaani, hiyo inatokana na namna anavyovaa, kwa kifupi kila unapokutana naye utamkuta kiselasela kwa maana ya kibegi mgongoni, mikato ya kupigilia vipensi na sendo, kichwani kwake anapenda kuvaa vikofia fulani hivi ameizingi ‘Amazing’.

Mwanaspoti linajua kufukunyua mambo, Chief ni baba wa watoto wanne aliyowataja kwa jina la Khanifa (13), Islam (9), Ramaki (6) na Muktari (3), ameliyewapa kwa mke wake mrembo, Riziki Ramadhan.

Anafichua akiwa nyumbani ni baba anayeipenda famili yake iwe na furaha na ifurahie uwepo wake na kuweka wazi furaha anayowapa mashabiki wa soka inaanzia katika familia yake.

“Unajua nini? Najichanganya kitaa kwa ajili ya kusaka mia mbili ya kuilisha familia yangu na sio kama mimi ni mhuni kama wengi wanavyodhani na ndio maana napambana ili watoto wangu wapate elimu, you know why Education is first for my children’.

“Sitaki waje waunge unge kama mimi baba yao ndio maana najitahidi kwa kila hali na hiki king’eng’e ninachoongea niwafundishe maana nilisoma zaidi ya miaka miwili English Course kuanzia mwaka 2002,”anasema.

Hapo patamu, Mwanaspoti likataka kufahamu kwa nini alienda kusoma English course! Anafunguka kama ifuatavyo “Nilipomaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Mtama mwaka 1998, iliopo Lindi ambayo amesoma na Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, sikubahatika kufaulu ndipo nikaamua kuingia jijini Dar es Salaam.

“Nilipofika Dar niliingia kitaa ili kujua ishu za kimaisha wanavyozifanya wenzangu, ndipo nilipokutana na lile kundi la vijana ambalo lina ndoto za kwenda Afrika Kusini, lakini wakasema ili ufanikiwe kufika huko lazima ung’eng’e uwe umekaa sawa kichwani.

“Nikaona isiwe tabu nikaingia darasani nikafanikiwa kusoma, lakini kwa bahati mbaya rafiki yangu aliyekuwa ananipa michongo ya kwenda Sauzi tukapoteana, ila nikapata bahati nyingine ya kuwa kiongozi kwenye kampuni moja ya Kichina mwaka 2005 iliyokuwa inatengeneza yeboyebo, kazi yangu ilikuwa ni kuwaunganisha wafanya kazi na mabosi,” anasema.

JINSI ALIVYOKUTA NA MKEWE

Safari ya uhusiano inasisimua kidogo ndani yake kuna vichekesho vya hapa na pale, mke wake alikuwa Mama Lishe Tandika karibu na maeneo ambayo alikuwa anafanya biashara zake, jamaa alikuwa anajifanya mteja wa kudumu, huku akimsifia mwanadada huyo kwamba anapika chakula kizuri, msafi na anayewajali wateja.

Anasimulia kuna wakati alikuwa anakosa noti, lakini alikuwa radhi kukopa ili mladi tu aonekane mwanaume maridadi mwenye noti mfukoni, huku lengo lake lilikuwa ni kumuona mrembo huyo mara kwa mara.

Kama unavyojua biashara ya mama lishe ina wateja wanaume na wanawake jamaa upendo ukaanza kumkolea ndani kwa ndani na kufikia hatua ya kuwa na ka-wivu fulani hivi, lakini alikuwa akimcheki mrembo huyo alikuwa hana hata dalili za kuonyesha kama anamuelewa hisia zake.

Jamaa akaona isiwe noma akamfuata dada wa mrembo huyo na kumwambia haja ya moyo wake, Mungu si Athumani mambo yake yakatiki, akiwa anaendelea kusimulia mwanamama huyo mwenye watoto wanne akadakia na kuelezea vitu alivyovifanya jamaa hadi kukubaliwa.

Anaanza kwa kicheko na kusema kuwa “Jamani tunatoka mbali yaani nikimwangalia mume wangu we acha tu, nilimpendea kitu kimoja, walikuwa wakija Mgambo katika biashara yangu basi anapambana mpaka nabaki salama, ndio maana aliponifuata nikamkubali kirahisi nikiamini ninaangukia mikononi salama na imekuwa hivyo.

“Ni baba mcheshi anayependa kucheza na familia yake, muda mwingi akiwepo tabasamu haliniishi mdomoni, anajali kwa kidogo anachokipata na ndio maana hata katika ushabiki wake sioni cha ajabu.

“Kikubwa huwa namwambia akiondoka nyumbani awe msafi, avae vizuri na nguo zake za kushangilia akavalie sehemu sahihi na sio atoke nazo hapa nyumbani, nafurahi kuwa na mwanaume maarufu, akianza kuongea kwenye redio mashoga zangu wanakuja kuniita kumbe mumeo wako msomi, kingereza kile anachoongea, laiti wangejua ameishia darasa la saba wasingesema yote,” anasema huku jicho la upendo likimtazama kidogo mume weka kisha anainamisha macho kidogo na kutabasamu.

NYUMBA YAKE

Mwaka 2014 alipata Shilingi 1.5 milioni kupitia kikundi cha ushabiki, lakini kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa mhamasishaji namba moja, akapewa Shilingi 500,000 ambazo ndizo alizonunulia uwanja ambao amejenga nyumba anayoishi.

“Mwaka 2015 nikaibuka shabiki bora na sio kikundi nikapewa Shilingi 300,000 nilipozipeleka kwenye timu wakaniambia nizitumie, ndipo nikaanza ujenzi nikiwa naungaunga na kidogo nilichokuwa napata mpaka hapo mnapoona,” anaonyesha na mpiga picha wetu, Michael Matemanga hakutaka kuchelewesha akafyatua picha za kutosha.

“Si hivyo tu, umaarufu unanisaidia kwa sehemu kwani sasa hivi silipi nauli magari ya kutoka Tandika kuja huku nyumbani, Chamazi yaani makonda na madereva wamekuwa marafiki wangu, lakini pia nimefahamia na viongozi wa serikali kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda Simon Siro ambao wanaweza wakanipa misaada mikubwa zaidi,”anasema

DILI LAKE NA NAPE LILIYEYUKA

Mwaka 2014, Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipoviona kwa mara ya kwanza vituko vyake alimuita ofisini kwake na kuanza harakati za kumtengezea paspoti ili awe anasafiri na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ popote ambapo ingeenda kutimiza majukumu yake.

“Wakati akiwa kwenye harakati hizo, Waziri Nape akaondolewa kwenye nafasi hiyo, hivyo sikuweza kuendelea na jambo hilo, lakini kwa kweli naipenda sana timu yangu ya taifa na akitokea mtu wa kunisaidia kupata pasipoti nipo tayari kuitumikia kwa upande wa kushangilia,” anasema.

MPINZANI WAKE KATIKA NDONDO

“Hata kama watakuja na vituko gani, hakuna mtu anayeweza kunifikia, hawawezi kuwa kama mimi, ndio maana hata mwaka huu nimepewa tuzo ya shabiki bora na kiasi cha pesa cha Sh 1 milioni,”anasema.

ODA ZA KAZI

Chief anasema uongozi wa Timu ya Reha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) tayari imempelekea ofa ya kufanya nao kazi “Ndio tupo kwenye makubaliano, huwa najiuliza sana kama hizi timu ndogo zinanifuata kwa nini timu ya taifa langu Taifa Stars hawaoni kama naweza kuhamasisha wakati vijana wetu wakifanya kazi,” anasema.

NDOTO YAKE

Anaweka wazi alikuwa anatamani siku moja kuwa mwanasoka mkubwa ndani na nje ya nchi, lakini ndoto yake haikuishi kutokana na ugumu wa maisha na alijikuta anakosa muda mwingi wa kujitoa.

Aliichezea timu yake ya mtaani inayojulikana kama Red Scorpion, iliopo Tandika wenyewe walikuwa wanaita cha ndimu, nafasi aliyokuwa anacheza ni ya kiungo mkabaji kwa sasa anajifananisha aina ya uchezaji wake na Jonas Mkude wa Simba.

“Sasa Ndondo Cup ilipoanza umri wangu ulikuwa umeenda nikaamua niibukie kwenye ushangiliaji, lakini enzi hizo niliupiga mwingi, huwa namwangalia sana Mkude laiti kama Mungu angenifikisha kwenye mafanikio hayo, basi nilikuwa na aina ya uchezaji wake,”anasema.

BIASHARA

Ameajiriwa na mtu kufanya biashara ya vibegi ambapo kwa siku inategemeana kuna wakati analipwa Sh8,000 wakati mwingine 7,000 akidai inafuatana na jinsi ambavyo biashara kwa siku hiyo imetoka.

“Nilikuwa na mtaji wangu nikaporomoka na ndio maana nikaamua kukubali kuajiliwa ili nipate pesa ya kuilisha familia yangu, ila baada ya kuwa maarufu tunapata wateja wengi ila ndio napata hicho kwa masaa manne ninayofanya kazi hiyo,”anasema.

USHIRIKINA VIPI

Anakiri mambo ya mpira yana vioja akidai mara mbili amewahi kwenda katika Makaburi ya Yombo Dovya kufukia vichwa vya kuku ili timu yake ya Kauzu FC iweze kushinda mechi ilikuwa dhidi ya Goms ya Gongo la Mboto na wakafanikiwa ila anakiri haikuwa poa kulala makaburi na kudai ilihitaji moyo wa kishujaa kama alivyofanya yeye.

“Niwe mkweli nimefanya kwa ajili ya timu lakini sio kama mimi mshirikina, kuna wakati mwingine uongozi wangu unaniambia kutokana na vituko ninavyofanya, basi wananipeleka kwa mtalamu ili nijilinde nimekuwa nikifanya.

“Lakini ile kupanda kwenye ungo, kwenda bila viatu kuchukua tuzo ya mwaka huu ilikuwa ni uhamasishaji na sio vingine, hii ni kazi lazima niwe mbunifu, nataka nieleweke hivyo,”anasema.

CHANGAMOTO

Anafichua asilimia kubwa ya wale ambao hawafahamu maisha yake kiundani basi wanamuona ameyapatia, lakini anawafahamisha bado anasota kusaka shilingi ya kumpendezesha mkewe na kufanya wanawe waende shule.

“Changamoto nyingine ni pale watu wanapochukulia mambo ya uwanjani na kuniona pengine mimi mshirikina, wajue tu nilipenda sana kucheza mpira na hasira zangu zikaishia kushangilia, ila watoto wangu sitaki kabisa waje kupenda ninavyofanya,” anasema.

MBWANA SAMATTA ANAMPA SALUTI

Anafichua kuna timu alikuwa anacheza staa wa Kitanzania anayekipiga KRC Genk ya Ubeligiji, Mbwana Samatta ipo Tandika ambapo anadai alimshuhudia namna alivyokuwa anajituma akiwa umri mdogo hivyo mafanikio yake yanatoa funzo kwake.

“Namjua alipotokea na ndio maana nampenda, kwani alianza kuonyesha juhudi, sasa ukimzungumzia ni staa wa kimataifa ila alianzia Tandika ambako wengine bado tunagangaganga maisha na hatuelewi hata tutokee wapi, ila kilichobakia ni kumshangilia kwa nguvu zetu zote,” anasema.