Usiku mzito Liverpool kwa Roma, Real na Bayern

Muktasari:

Salah anatazamiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Jurgen Klopp itakapocheza na timu yake ya zamani ya Roma, katika nusu fainali ya kwanza inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali huko Anfield leo Jumanne.

Liverpool, England. Liverpool ya Mohames Salah leo watakuwa na kibarua kizito mbele ya AS Roma katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa kwenye Uwanja wa Anfield.

Salah anatazamiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Jurgen Klopp itakapocheza na timu yake ya zamani ya Roma, katika nusu fainali ya kwanza inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali huko Anfield leo Jumanne.

Kesho, Jumatano kutakuwa na kipute kingine, ambapo vigogo Bayern Munich watakuwa nyumbani Allianz Arena kumkaribisha Cristiano Ronaldo na chama lake la Real Madrid.

Itakuwa wiki kali na hakika usithubutu kupitwa. Liverpool wametinga hatua hiyo baada ya kuwasukuma nje Manchester City kwa mabao 5-1, huku ushindi wao ukichagizwa zaidi ya Mo Salah, lakini AS Roma nao si wa kubeza baada ya kupindua matokeo dhidi ya Barcelona na sasa wametinga nusu fainali.

Bayern na Real Madrid ni mechi ambacho mashabiki wamepata kushuhudia mara kadhaa zikimenyana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini safari hii mechi yao inatazamwa kwa mtazamo tofauti.

Madrid wanaamini staa wao Ronaldo ataendelea kuwavusha kwenye vizingiti vizito katika kutimiza ndoto yao ya kubeba taji hilo kwa msimu wa tatu mfululizo.