Usibishe Bocco, Okwi kumaliza kazi

Muktasari:

Ushindi wa Simba leo utamfanya Djuma awe katika mazingira salama kuliko kupoteza ama kutoka sare kwa mechi hiyo kwani wakipoteza mwisho wake wa kuwepo ndani ya Simba utakuwa mbaya

MTWARA.Simba leo Jumamosi kitakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Ndanda katika mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara. Simba itaingia uwanjani kusaka ushindi wa tatu mfululizo baada ya kuchomoza na ushindi kwenye mechi mbili za kwanza dhidi ya Tanzania Prison na Mbeya City ambazo walicheza Uwanja wa Taifa.
Katika mechi hizo Simba walishinda mabao matatu ambayo yakifungwa na straika matata Meddie Kagere.
Kikosi cha Simba kilifanya mazoezi mapesi ya mwisho jana katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini hapa, ambapo Kocha wa Simba Patrick Aussems amewaka mipango yake hadharani kuwa pointi tatu ndio wamezifata katika mechi hii na si jambo lingine.
"Kikosi changu kipo kamili na uwepo wa mastraika wangu Kagere,  Bocco na Okwi tena wakiwa fiti ni jambo zuri, ingawa hawajabatika kucheza pamoja ingawa mechi hi wana nafasi ya kucheza wote.
"Kagere amefunga mabao matatu katika mechi mbili za ligi kwahiyo atacheza kwa kujiamini na kubwa zaidi atakuwa na kiu ya kuendelea kufunga.  Bocco katika mechi mbili zote amecheza lakini hajafunga na Okwi hajacheza hata mechi moja kwa kuwa majeruhi kwa maana hiyo nawapa nafasi kubwa ya kufunga katika mechi hii," alisema.
Wakati Aussems akitamba kupata ushindi kupitia nyota wake hao, kiungo wa Ndanda nao wametamba kubaki na ushindi nyumbani.
"Ndanda hii imebadilika baada ya usajili uliofanywa msimu huu, tumedhamilia kuvunja rekodi, tunafahamu tunacheza na timu kubwa ambayo hutajawahi kuvuna pointi tatu dhidi yao lakini mechi hii tutapambana mpaka kuhakikisha tunachukua pointi tatu dhidi hao kwani hakuna timu ambayo inakwenda vitani wakiamini kushindwa, " alisema Idrissa Bandari, Ofisa Habari wa Ndanda.

REKODI ZAINYIMA USHINDI  NDANDA
Ndanda FC wamepanda kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2014/15 hawajawahi kuifunga Simba hata mara moja.
Ndanda dhidi ya Simba wamekutana mara nane,  nyumbani na ugenini ambako wamecheza mechi nne nne,  ambapo mara zote Simba huondoka kifua mbele.
Mwanaspoti inakuletea mechi zote ambazo Ndanda tangu wamepanda hawajambulia hata pointi tatu dhidi ya Simba.

2014/15
Huu ulikuwa ni msimu wao wa kwanza kukutana na Simba ambapo mzunguko wa kwanza mechi ya kwanza ilichezwa uwanja wa Nangwanda. Mechi hiyo ilichezwa Januari 17 Ndanda walipokea kipigo cha mabao 2-0.
Mechi ya pili ilichezwa uwanja wa Taifa ambapo Simba waliendeleza ubabe wa mabao 3-0 mechi iliyochezwa Aprili 25.
Msimu huo ambao Ndanda walimaliza nafasi ya tisa kwa kufikisha pointi 31 walifungwa mabao matano huku wakishindwa kupata bao hata moja.

2015/16
Msimu huu ulikuwa wa pili kwa Ndanda ambao walimaliza Ligi wakiwa na pointi 35 na kushika nafasi ya ya tisa huku wakiendeleza unyonge mbele ya Simba. Mechi ya kwanza ambayo ilichezwa siku ya kwanza ya mwaka 2016 katika raundi ya sita Ndanda wakiwa nyumbani walifungwa bao 1-0.
Mechi ya marudiano iliyochezwa Machi 10, Simba wakiwa uwanja wa Taifa waliibuka na ushindi wa bao 3-0, msimu huo Ndanda ilifungwa mabao manne katika mechi mbili baada ya kupoteza mechi ya nyumbani na ugenini.

2016/17
Msimu huu Ndanda walimaliza Ligi wakishika nafasi ya 13 kwa kukusanya a pointi 33 huku Simba wakimaliza nafasi ya pili wakipoteza ubingwa hatua za mwisho dhidi ya Yanga ambao walimaliza pointi sawa lakini wakiwa na idadi ndogo ya magoli ya kufungwa na kufunga. Mechi  ya kwanza iliyochezwa uwanja wa Taifa, Simba waliifunga Ndanda mabao 3-1, Agosti 20.
Ndanda kwa mara ya kwanza na ya mwisho kabla ya mchezo wa leo kufunga bao la pekee dhidi ya Simba katika matokeo ya mechi hiyo.
Mechi ya pili ambayo ilichezwa Nangwanda Sijaona Ndanda walikubali kuwa wanyonge dhidi ya Simba baada ya kufungwa tena mabao 2-0,  Desemba 18.
Katika mechi mbili za msimu huo, Simba walichukua pointi sita kama kawaida lakini walifunga mabao matano na wao walifungwa moja.

2017/18
Msimu uliopita ambao Simba walitwaa ubingwa kwa kishindo kwa kupoteza mechi moja tu dhidi ya Kagera Sugar waliwafunga Ndanda mechi zote mbili.
Ndanda ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya 14 baada ya kukusanya pointi 29, mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa uwanja wa Nangwanda ikiwa chini ya Masoud Djuma walishinda bao 2-0, mechi ilichezwa Desemba 30. Mabao yote ya Simba yalifungwa na John Bocco.
Mei 6 ndio ilikuwa siku ya Simba kucheza dhidi ya Ndanda ambao walifungwa tena bao 1-0. Mechi ya leo Jumamosi chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems itakuwa ya tisa kwa Ndanda kukutana na Simba tangu wapande Ligi Kuu huku Simba wakitaka kuendeleza rekodi wakati Ndanda wakitaka kuvunja rekodi kwa kupata ushindi kwa mara ya kwanza wakiwa nyumbani.

MECHI YA KUMBEBA DJUMA
Kuna kila dalili kwamba mwisho wa kocha msaidizi Masoud Djuma umekaribia ndani ya Simba baada ya kuachwa jijini Dar es Salaam wakati timu yake ikiwa kwenye kibarua kigumu cha ugenini, lakini Djuma huenda anafanya sara zote ili Simba ishinde mechi hiyo.
Dua za Djuma ni baada ya kuwepo na tuhuma za kuwagawa wachezaji ndani ya Simba ili wafanye vibaya na kocha mkuu Aussems aonekana uwezo wake ni mdogo
Djuma aliwekwa kitimoto na viongozi wa Simba ambao sasa wanafanya uchunguzi wa kimya kimya kubaini ukweli wa tuhuma zote walizozitapa juu yake.
Ushindi wa Simba leo utamfanya Djuma awe katika mazingira salama kuliko kupoteza ama kutoka sare kwa mechi hiyo kwani wakipoteza mwisho wake wa kuwepo ndani ya Simba utakuwa mbaya.
Yeye anasema; "Hakuna mtu ambaye anaomba mabaya kwake ama kwa timu, sina ujanja wowote wa kuwashawishi wachezaji wacheze chini ya kiwango, wachezaji wa Simba ni wazuri na naamini wapo kwa ajili ya kuipambania Simba na si mtu mmoja, nimebaki kwa ajili ya kuendelea na programu aliyoniachia kocha mkuu."