Ushindi washusha presha Kagera Sugar

Muktasari:

Timu hiyo ilianza msimu kwa kutoshinda katika michezo yake sita ya mwanzo ya Ligi Kuu

Mwanza. Ushindi walioupata ugenini Kagera Sugar dhidi ya ndugu zao, Mtibwa Sugar jana Jumapili, umeamsha morali yao na kuahidi kuendeleza vichapo kwa kila mchezo.

Kagera Sugar aliyoanza msimu vibaya kwa kucheza mechi sita bila ya kushindi ilipata ushindi ugenini kwa kuwafunga Mtibwa Sugar kwa bao 1-0 ugenini.

Ushindi huo umefanya Kagera Sugar kufikisha pointi 10, na kupanda hadi nafasi ya 10, pamoja na kuvunja rekodi ya Mtibwa  Sugar ya kucheza tisa za Ligi Kuu msimu huu bila kupoteza.

Kutokana na ushindi huo, benchi la ufundi limesema sasa wanajiandaa kuhakikisha kila timu wanayokutana nayo inalamba kisago ili kujiweka nafasi nzuri.

Kocha Msaidizi wa Kagera, Ally Jangalu alisema licha ya ushidani uliopo kwa kila timu kusaka pointi tatu, watahakikisha wanalinda ushindi kwa michezo iliyobaki.

“Haikuwa kazi ndogo kupata ushindi dhidi ya Mtibwa, tunawapongeza vijana wetu kupambana kutimiza malengo, sisi benchi la ufundi tutaendelea kujipanga kwa mechi zinazokuja,” alisema Jangalu.