Alichosema Wambura kesi ya Malinzi

Muktasari:

Ofisa Mtendaji Mkuu Wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira Wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura (49) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Muhtasari wa  Juni 5, 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za benki za TFF zilizopo Stanbic benki  ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu Wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira Wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura (49) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Muhtasari wa  Juni 5, 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za benki za TFF zilizopo Stanbic benki  ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.

Wambura ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka aliyaeleza hayo leo Jumatatu wakati akiongozwa na Wakili Wa Serikali, Shadrack Kimaro kutoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais Wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi pamoja na wenzake wanne.

Akitoa ushahidi kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wambura alidai kuwa anasema hayo kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha Juni 5, 2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa  benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.

Alidai kuwa Edgar Masoud alikuwa ni Mkurugenzi Wa Fedha na Utawala TFF lakini kwa sasa ni marehemu na kwamba alifariki mwaka 2017.

Akitoa  ushahidi huo Wambura alidai kuwa  mchakato ulitakiwa kupelekwa kama ajenda ukieleza sababu za kutaka kufanya mabadiliko ya watia saini katika kamati tendaji ambapo ikiridhia mabadiliko hayo yanafanyika.

Alibainisha kuwa baada ya kupitishwa kwa mapendekezo hayo ina  maana muhtasari huo unaenda kuitishwa katika kikao kinachofuatia kwa ajiri ya kuthibitishwa kuwa ndiyo uamuzi uliofanyika.

Awali 

Shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka alidai  kuwa yeye alikiwa Ofisa Mtendaji Mkuu Wa Bodi ya Ligi tangu Juni 2015 na majukumu yake yalikuwa ni kusimamia shughuli za ligi pia ni mjumbe sekretarieti ya TFF ambayo inawezesha vikao vya kamati tendaji  kufanyika.

Wambura alidai kuwa kwa mujibu wa katiba ya  TFF  vikao  vinne  vinatakiwa kufanyika kwa mwaka na pale inapotokea dharura, panapotokea mahitaji.

"Mwaka 2016 kamati tendaji   ilikuwa na wajumbe wasiopungua 20 na wasiozidi 24 na kwamba utaratibu wa ufanyaji vikao kinaitwa na Mwenyekiti na kuwapelekea ajenda wajumbe," alieleza Wambura.

Alidai kuwa nyaraka za ajenda zinaandaliwa na sekretarieti chini ya katibu mkuu na rais ambaye ndiyo msimamizi wa sekretarieti.

 Wakati vikao vinafanyika sekretarieti chini ya katibu mkuu inachukua muhtasari ambao unawasilishwa katika kikao kinachofuata kwa ajili ya kuthibitishwa na kusainiwa na mwenyekiti ambaye ni rais  wa TFF,  ama makamu wa rais.

Alidai 2016 aliyekuwa Mwenyekiti ni Jamali Malinzi  hata hivyo Wakili Kimaro alimwonyesha shahidi huyo  muhtasari wa Juni 5,2016 ukimwonyesha yeye ni miongoni mwa wajumbe wa sekretarieti waliohudhuria katika kikao hicho.

Baada ya kuonyeshwa na kupitia muhtasari huo, Wambura alidai kuwa muhtasari huo wa Juni 5,2016 umeghushiwa na kwamba yeye haufahamu  kwa sababu alikuwepo katika hicho kikao na kwamba hakukuwapo na ajenda kubadilisha watia saini wa TFF.

Akihojiwa na mawakili wa utetezi 

Wambura alidai kuwa wakati Jamali Malinzi akiwa rais  wa TFF yeye alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 2 milioni na   baada ya kuondoka madarakani hivi sasa analipwa mshahara wa Sh 7 milioni.

Wambura alieleza hayo baada ya kuulizwa na Wakili Rweyongeza kuwa aliwahi kupeleka maombi ya kuongezwa mshahara kwa Malinzi, Wambura alidai kuwa hakumbuki, aliulizwa wakati Malinzi yupo madarakani ulikuwa unapata kiasi gani:

 

Wambura :Sh 2 milioni 

Rweyongeza: Ulipeleka maombi upate Sh 7 milioni kwa mwezi kwa  Malinzi akakukatalia.

Wambura: Sikumbuki

Rweyongeza: Ni kweli wakati Malinzi akiwa madarakani alikataa nyongeza hiyo?

Wambura: Siyo kweli.

Rweyongeza: Sasa hivi ni kweli unapata Sh 7 milioni kwa mwezi?

Wambura : Ni kweli.

 

Rweyongeza: Hizi  Sh 7 milioni  zimeidhinishwa na rais wa sasa wa TFF baada ya kutoka Malinzi madarakani?

Wambura: Ni kweli.

Rweyongeza: Kwa mantiki ya kawaida chini ya rais wa zamani na wa sasa wewe upo vizuri zaidi.

Wambura: Nipo vizuri kikazi.

Rweyongeza: Mshahara wa  Katibu Mkuu  Wa TFF unaufahamu?

Wambura: Siufahamu.

Rweyongeza: Bodi ya Ligi ipo chini ya TFF nikisema Katibu Mkuu Wa TFF ni mkubwa kwako.

Wambura: Ni sahihi.

Rweyongeza: Una habari unamzidi mshahara?

Wambura: Sina  habari.

Rweyongeza: Unaweza kutaja nyazifa ulizopitia TFF 2011 na 2013?

Wambura:  Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF,  TMS Meneja, Mkurugenzi Wa Mashindano na niliwahi kukaimu Ukatibu Mkuu wa TFF Novemba 2013 hadi Desemba 31,2013.

Rweyongeza: Wakati huo nani walikuwa watia saini wa TFF?

Wambura:  Boniface Wambura, Jamali Malinzi,  Wallace Karia na Yonaza Seleki  na kwamba wakati anakaimu ukatibu Mkuu TFF alikuwa mtia saini.

Rweyongeza: Kamati tendaji ni kikao gani kilikaa kuwateua nyie kuwa watia saini wa TFF.?

Wambura: Sikumbuki.

Rweyongeza: Na wewe ndiyo ulikuwa  katibu wa  kukuteuwa wewe mwenyewe kuwa mtia saini na wenzako?

Wambura: Ni kweli nilikuwa katibu wa vikao vyote.

Rweyongeza: Wewe ndiyo uliyejaza fomu za kwenda benki kubadilisha mtia saini wa benki kama katibu mkuu Wa TFF

Wambura: Sikumbuki.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 28 na 29 , mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

 

Katika kesi hiyo washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi (57), Katibu Mkuu wa TFF,  Mwesigwa Joas Selestine (46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga (27).

Meneja wa  Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF,  Flora Rauya.

 Kwa pamoja wanakabiliwa na  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 ambapo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 30.

Katika mashtaka hayo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na Sh 43,100,000.

Mwesigwa anakabiliwa na mashtaka sita  ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  na utakatishaji wa fedha.

Kwa upande wa mshtakiwa Nsiande anakabiliwa na mashtaka mawili ya utakatishaji wa fedha, mshtakiwa  Zayumba yeye  anakabiliwa na mashtaka  tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shtaka moja la kughushi. 

Washtakiwa walikana mashtaka yanayowakabili, Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.