NINACHOKIAMINI: Usajili wa Yanga, Simba na maisha ya kimjini mjini

Muktasari:

Mjini hakuna tamaduni, hakuna mila na desturi, hakuna upendo wala ushirikiano, badala yake watu wanaishi kwa fasheni bila kujali kama kuna uhalisia.

MAISHA ya mjini ya ajabu sana, huwa yanabadilika kila dakika na kila siku watu wanakuja na staili tofauti ya maisha. Achana na foleni za Dar es Salaam, tena usipende kukumbuka joto lake.

Mjini hakuna tamaduni, hakuna mila na desturi, hakuna upendo wala ushirikiano, badala yake watu wanaishi kwa fasheni bila kujali kama kuna uhalisia.

Usishangae kuona mtoto wa miaka miwili akifanyiwa sherehe ya bethidei ya Sh20 milioni, wala usije ukazimia ukiona mwanafunzi anayemaliza darasa la saba akifanyiwa sherehe ya Sh50 milioni.

Staili ya maisha ya mijini huwa kama upepo unaovuma kutoka nyumba moja kwenda nyumba nyingine, kutoka familia mmoja kwenda familia nyingine na hatimaye jamii yote hujikuta ikiishi kwa staili fulani ya maisha. Staili ya maisha hubadilika mara kwa mara.

Staili ya maisha ya mijini imekuwa ni ya kuigana zaidi kuliko uhalisia. Maisha haya yamekuwa yakifuata mkumbo au kwa kifupi unaweza kusema yamekuwa yakitawaliwa na mihemko na upepo wa kipindi husika.

Unadhani hali hiyo ipo katika maisha ya kawaida tu? Hapana. Hata kwenye sekta za michezo hasa soka hilo ndilo linalotawala hasa katika klabu kongwe nchini Simba na Yanga.

Yanga walikuwa na kocha aliyewapa vikombe mbalimbali, Hans Pluijm lakini wakamtosa na kuachana naye kwa sababu tu, Simba ilikuwa na kocha wa Cameroon, Joseph Omog.

Inawezekana kuna mtu mmoja Yanga aliibuka na kusema ‘Tukitaka kuwamaliza Simba inabidi tuwe na kocha wa Zambia’, baada ya hapo akapigiwa makofi na uamuzi ukapitishwa.

Hakuna sababu yoyote ambayo Yanga wanaweza kujitetea zaidi ya hilo. Sijawahi kuwauliza, lakini kwa sababu wametoa nafasi ya kila mtu kufikiria anachotaka, sijaona dhambi kuwa na mtazamo huo.

Tupo katika kipindi cha usajili wa wachezaji. Tutashuhudia mambo mengi wakati huu, Simba watasajili wachezaji wengi na Yanga pia watafanya hivyo hivyo.

Makocha watakabidhi mahitaji ya timu zao, lakini wachezaji watakaosajiliwa watakuwa ni zaidi ya hao. Mahitaji ya kocha kwa Simba na Yanga huwa si jambo la msingi sana.

Suala la msingi ni mashabiki wanataka nini na sio kocha anataka nini? Mashabiki siku zote huwa hawafikirii kiuhalisia, husukumwa na mihemko na kuigana.

Kama Yanga watasajili mchezaji wa Nigeria, basi Simba watataka wasajili Ghana. Yanga ikisajili Kenya, Simba watataka kwenda Uganda. Hayo ndio maisha ya klabu hizi kubwa mbili, hawana tofauti sana na maisha ya mjini.

Kama jinsi maisha ya mjini yanavyotafuta umaarufu zaidi, ndivyo ilivvyo pia kwa klabu hizo.

Simba wakisajili mchezaji kwa Sh50 milioni, Yanga watataka kusajili kwa Sh70 milioni. Lengo ni kutafuta nani maarufu.

Azam ni miongoni mwa klabu ambayo nilikuwa naikubali sana. Walianza kisayansi, ilikuwa inasimamiwa na kampuni, walijenga uwanja maridadi na hakika ilikuwa ni sawa na timu kutoka nchi zilizopiga hatua ya soka.

Hata timu nyingi za Afrika Kusini hazina viwanja.

Lakini walipoingia watu wanaojiita wa mpira Azam, wakaingizwa mambo ya mjini, wakajikuta wameingia kwenye mtego wa Simba na Yanga. Wakasahau sayansi, wakaanza kuendesha timu kiswahili.

Leo wameshtuka wakiwa wamechelewa, wamefuta baadhi ya vyeo katika klabu hiyo, wamekataa kulipa wachezaji mishahara mikubwa, wamekataa kusajili wachezaji kwa pesa na ndio maana tunaona wachezaji wengi wanaondoka wakiongozwa na John Bocco.

Na hilo ni jambo la msingi, Azam hawakutakiwa kuishi kama Simba na Yanga, walifanya kosa. Waache Simba na Yanga waishi kimjini, wao Azam waishi kisayansi.

La msingi zaidi viongozi wa soka wanatakiwa kubadilika na kuishi maisha ya uhalisia tofauti na sasa, vinginevyo soka hili litakuwa linapiga hatua 10 mbele wanarudi 15 nyuma.