Simba: Usajili huu temeni mate chini

UONGOZI wa Simba umesisitiza kwamba usajili walioufanya kwa ajili ya msimu mpya wamedhamiria mambo makubwa wala hawabahatishi na anayebisha atajionea mwenye Uwanja wa Taifa kitakachotokea.

Makamu Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ameliambia Mwanaspoti jana Jumatatu kwamba kikosi walichosajili mpaka kufikia dakika hii kina uwezo wa kutwaa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo.

“Yaani hiki kikosi ambacho tumesajili mpaka sasa hivi kina uwezo wa kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo bila wasiwasi wowote na hapo bado hatujamaliza. Kimsingi mwisho wa mwezi huu ndiyo tunamaliza kila kitu tunaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

“Katika hizo mechi za kujiandaa ambazo tutakuwa tunafanya kama kocha akiona kwamba kuna sehemu panahitaji mabadiliko tutafanya kwa haraka bila kupoteza muda, tunataka kuwa na kikosi chenye hadhi ya Simba ambacho kwa kipindi kirefu tulikipoteza,” alisisitiza Kaburu, mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.

Usajili mkubwa ambao mashabiki wa Simba wanausubiri kwa sasa ni ule wa straika Mzimbabwe, Donald Ngoma, ambaye viongozi wa Simba wanafanya naye mazungumzo kwa ukaribu ingawa inadaiwa kwamba Yanga na wao wameshamalizana naye. Ngoma imeripotiwa kwamba anatua nchini leo. Mbali na huyo, Simba imemalizana na Emmanuel Okwi ambaye tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili na tajiri wa Simba, Mohammed Dewji, amesema hiyo ni zawadi Idd kwao.