United yapambana na rekodi ya Van Dijik

DAKIKA za majeruhi katika dirisha la uhamisho pale England. zimebakia saa 72 tu kabla ya dirisha hilo kufungwa na Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anapambana na rekodi ya uhamisho kwa mabeki, iliyowekwa na mlinzi wa Liverpool, Virgil Van Dijik Januari.

United juzi ilichapwa bao 1-0 na Bayern Munich pale Ujerumani na Mourinho anadaiwa kuelekeza akili yake zaidi kwa mlinzi wa Leicester City, Harry Maguire na anaweza kuweka mezani dau ambalo litavunja rekodi ya uhamisho ya mabeki.

Leicester wanataka zaidi ya Pauni 75 milioni ambazo Liverpool ilitumia kumnunua Van Dijik dirisha la Januari akitokea Southampton na United wanaonekana kuhaha kumnunua Maguire kwa dau lolote lile kutokana na ukame wa walinzi wa kati unaowakabili.

Muda wowote kuanzia sasa wataweka dau hilo kwa Maguire kabla ya pambano lao dhidi ya Leicester City kwa ajili ya kumzuia staa huyo wa kimataifa wa England kucheza pambano hilo la ufunguzi wa Ligi Kuu siku ya Ijumaa usiku.

Awali United walihamia kwa mlinzi, Yerry Mina wa Barcelona lakini dili hilo lilivunjika kutokana na utata uliojitokeza kati ya United na wakala wake na taarifa zinadai sasa staa huyo wa kimataifa wa Colombia ataenda Everton kwa dau la pauni 28 milioni.

United pia walihamia kufanya mazungumzo na Bayern Munich wakiangalia uwezekano wa kumchukua mlinzi, Jerome Boateng ambaye ni staa wa zamani wa Manchester City, lakini akili kubwa kwao inabakia kwa Maguire ambaye ndiye kwanza ameripoti katika kambi ya mazoezi ya Leicester baada ya mapumziko marefu aliyopewa kutokana na kushiriki michuano ya Kombe la Dunia.

Mlinzi huyo wa zamani wa Hull City aling’ara katika Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia na Leicester watapata mara nne zaidi ya pesa ambayo walitumia kumnunua kutoka Hull miezi 12 iiyopita wakati walipolipa dau la Pauni 20 milioni tu.

Kocha wa United, Jose Mourinho amepania kununua mlinzi wa kati kabla ya Ijumaa kutokana na kutowaamini walinzi wake wanne wa kati, Victor Lindelof, Phil Jones, Eric Baily na Marcos Rojo. Wote wamekuwa na matatizo tofauti.

Baily ambaye ni staa wa kimataifa wa Ivory Coast alikuwa hapangwi na Mourinho katika mechi za mwisho za msimu bila ya sababu inayoeleweka lakini pia alisumbuliwa na majeraha kwa kipindi kirefu na kuiacha safu hiyo shakani.

Staa huyo pia aliumia katika pambano la juzi na kushindwa kuendelea kitu ambacho kinaweza kumfanya Mourinho azidishe kasi katika kumnasa Maguire. Kwa upande wa Lindelof, mlinzi huyo wa kimataifa wa Sweden ameshindwa kumudu kasi ya Ligi Kuu ya England ikiwa ni msimu mmoja tu tangu anunuliwe kutoka Benfica ya Ureno.

Smalling na Jones ambao walicheza mara nyingi zaidi msimu ulioisha wamashutumiwa kwa kucheza chini ya viwango, hasa Smalling ambaye alichemsha kiasi cha kushindwa kuwepo katika kikosi cha timu ya taifa ya England kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.

Mara baada ya pambano la juzi, Mourinho alidai mashabiki wa United watarajie msimu mgumu kama timu hiyo itashindwa kununua mchezaji yeyote hadi kufikia Ijumaa wakati dirisha la uhamisho litakapofungwa.

“CEO wangu anajua ninachokitaka kwa muda mrefu. Anajua ninachotaka. Najua anajaribu kufanya jambo bora kwangu kwa muda mrefu na nina siku chache za kusubiri kitakachotokea.

“Klabu nyingine ambazo zinashindana na sisi zimekuwa imara na zina vikosi bora, kama vile Chelsea, Tottenham au Manchester City, au nyingine kama Liverpool imewekeza sana. Wananunua chochote na kila mtu. Kama hatutaiimarisha timu yetu basi tutarajie kuwa na msimu mgumu sana.”