Unadhani mchezo! Mastaa Simba wapagawa

Muktasari:

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, mastaa hao wa Msimbazi wameeleza walivyopokea taarifa hizo kwa furaha na kuona mwaka huu umekuwa wa neema kwao.

KUNA mtu anayeweza kusema hapendi kukutana na Rais wa nchi? Basi hata mastaa wa Simba wamepagawa baada ya kusikia Rais wa Tanzania, John Magufuli, ndiye atakayewakabidhi kombe na medali zao za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, mastaa hao wa Msimbazi wameeleza walivyopokea taarifa hizo kwa furaha na kuona mwaka huu umekuwa wa neema kwao.

Winga wa timu hiyo, Shiza Kichuya alisema Rais Magufuli kuacha shughuli zake ili aende uwanjani kuwakabidhi taji la ubingwa si jambo dogo bali inaonyesha ametambua kazi yao.

“Kwangu ni rekodi ya kipekee, rais kutukabidhi kombe! Nahisi nimeongeza kitu kikubwa katika kazi yangu ya soka, hivyo itabakia kuwa kumbukumbu nzuri,” alisema Kichuya anayeichezea Simba kwa msimu wa pili sasa.

Naye beki Salim Mbonde alisema anatamani kuvaa medali ya Ligi Kuu na kwa bahati mambo yamejipa, tena watapewa na Rais wa nchi, kitendo alichodai hakitafutika kichwani mwake.

“Kwangu ni faraja ya aina yake, Mkuu wa nchi kutukabidhi ubingwa si kitu kidogo, najisikia mwenye thamani kubwa na kwamba kujikita na soka kumbe sijapotea njia kutua Msimbazi,” alisema Mbonde.

Kwa upande wa Ally Shomary, alisema haamini mpaka atakapoona Magufuli anawakabidhi ndoo hiyo ya ubingwa ndio furaha yake itakapokuwa kubwa zaidi kuliko aliyonayo sasa.

Naye John Bocco alisema kwake anauchukulia kama ni msimu wa kihistoria.

“Nadhani kila mchezaji ambaye timu yake inashiriki Ligi Kuu Bara, alitamani angekuwa Simba ili aweze kupata baraka za Rais, si kitu kidogo hata nisingekuwa ndani ya klabu hii ningetamani kwani ni cha kuthamini kazi zetu,” alisema Bocco aliyefunga mabao 98 katika ligi hiyo kwa misimu 10 ya kucheza kwake tangu mwaka 2008.