Unaambiwa urembo unamtesa Kylie Jenner

Muktasari:

Kitendo hicho kimetafsiriwa kama harakati za mrembo huyo kutaka kurudi kwenye usichana haraka kwa kutumia vifaa ambavyo ni hatari kwa mwanamke aliyejifungua.

KINDA kutoka kwenye familia ya Kardashian, Kylie Jenner amejikuta akishambuliwa kutokana na kuvaa mkanda mzito wa kubana tumbo ikiwa ni miezi miwili baada ya kujifungua.

Kitendo hicho kimetafsiriwa kama harakati za mrembo huyo kutaka kurudi kwenye usichana haraka kwa kutumia vifaa ambavyo ni hatari kwa mwanamke aliyejifungua.

Siyo tu yeye, wasichana kibao wanapenda kurudia usichana kwa kufanya mambo mengine yanayohatarisha maisha, eti wapendeze.

Mtaalamu wa afya uzazi kutoka Texas, Dk. Cynthia Robins alisema mkanda huo ni hatari kwa afya ya Kylie.

Alisema kwa muda ambao Kylie ametoka kujifungua kiafya hatakiwi kuubana sana mwili wake.

“Ule mkanda ni mzito na unabana sana unaweza kwenda kubana maeneo mwingine ndani ya tumbo na kwenye nyonga ambayo hayatakiwi kubanwa ndani ya muda mfupi hivyo,”

Inadaiwa kuwa wakati qa ujauzito Kylie aliongezeka uzito jambo ambalo hakulifurahia hata kidogo.

Kwa sasa mrembo huyo anayeongoza kwa utajiri katika familia ya Kardashian anafanya kila linalowezekana kuhakikisha uzito wake unapungua na anarejea kwenye muonekano wake wa zamani.

Huenda Kylie ana lengo la kufuata nyayo za Dada yake Kim Kardashian ambaye licha ya kuzaa watoto wawili bado ni miongoni mwa mastaa wanaosifika kwa urembo duniani.