Umitashumta wakosa gari la kubeba wagonjwa viwanjani na kuweka hatarini maisha ya wanafunzi

Muktasari:

  • Kukosekana kwa magari ya kubebea wagonjwa yemesababisha kuanza kutumika magari ya kawaida kupeleka majeruhi hospitalini, tofauti na ilivyokuwa kwenye Umisseta.

Uwepo wa gari moja la kubebea wagonjwa ‘Ambulance’, limeweka hatarini maisha ya wanafunzi 2522 wanaoshiriki mashindano ya Umitashumta yanayoendelea jijini Mwanza.

Kukosekana kwa magari ya kubebea wagonjwa yemesababisha kuanza kutumika magari ya kawaida kupeleka majeruhi hospitalini, tofauti na ilivyokuwa kwenye Umisseta.

MCL Digital ulishuhudia mchezaji mmoja ambaye hakufahamika jina aliumia na kukosa huduma ya kwanza na kupelekwa hospitali kwa kutumia gari la kawaida.

Akielezea changamoto hizo, Mwenyekiti wa michezo ya Umitashumta kitaifa, Jeshi Lupembe alikiri kuwapo kwa mapungufu hayo na kusema tatizo ni kukosa udhamini.

Alisema kuwa mashindano hayo yana gari moja la kubebea wagongwa, hivyo likiwa halipo huamua kutumia magari ya kawaida ili kuhakikisha majeruhi anapata huduma.

“Kumbuka mashindano haya (Umitashumta) hayana mdhamini kama yalivyokuwa ya Umisseta, kwahiyo tunaamua kujichanga wenyewe na kutumia magari haya ya kawaida”alisema Lupembe.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo yeye na Maofisa Elimu Mikoa wameazimia kila Mkoa unapokuwa unacheza, gari la Afisa Elimu Mkoa husika lazima liwepo karibu.