Ukipanda basi la Man United hushuki

Muktasari:

Hii ndio tofauti ya kuchezea Man United na timu nyingine. Mchezaji unabembelezwa na kutengenezewa maisha ya kustarehe hata kama utakuwa kwenye basi la kukubeba kwenda uwanjani.

KUMBE basi la Manchester United ni zuri hivi, ndio maana wanataka kulipaki muda wote.

Kwa mastaa wa timu hiyo wanaopenda starehe kama Paul Pogba, Marcus Rashford na Romelu Lukaku watahitaji kukaa ndani ya basi hilo muda mwingi kuliko uwanjani.

Hii ndio tofauti ya kuchezea Man United na timu nyingine. Mchezaji unabembelezwa na kutengenezewa maisha ya kustarehe hata kama utakuwa kwenye basi la kukubeba kwenda uwanjani.

Basi hilo lililowagharimu Man United, Pauni 400,000, Van Hool TDX27 ASTROMEGA lilitengenezwa na kupambwa na kampuni ya Kibelgiji.

Ndani kuna vitu vingi vinavyovutia, vinavyowafanya wachezaji kuburudika wanapokwenda au kurudi kwenye mechi.

Likiwa na kimo cha futi 13 na urefu wa futi 46.27 na upana wa futi 8.36, basi hilo linapopita lazima utakodoa macho tu kulishangaa. Limejengwa kama ghorofa. Chini kuna siti zinazotosha wachezaji tisa na juu siti za kuketi wachezaji 29. Siti zake ni laini unapozikalia, ukiketi mwili unakuwa kwenye hali nzuri kwelikweli, huwezi kuhisi uchovu na zime zimetengenezwa Italia.

Ndani ya basi hilo, kuna televisheni 45 nyuma ya siti na nyingine zimewekwa kwa juu. Ni chaguo la mchezaji mwenyewe tu kama kutazama Netflix, DVD au vipindi vya kawaida tu vya televisheni na zimeunganishwa na Sky.

Ndani ya basi huko kuna intaneti ya WiFi, hivyo wachezaji wanapata burudani wanayohitaji. Basi hilo lina jiko pia na kunapatikana oveni mbili za NEFF, kila moja thamani yake ni Pauni 770 na microwave ya Panasonic yenye thamani ya Pauni 630 na mashine ya kutengenezea kahawa, Kenco yenye thamani ya Pauni 540.

Jikoni pia kuna friji, sinki la maji ya moto na mambo mengine yanayohusu mapishi.

Pia kuna bafu lililotengenezwa kwa staili ya kama kwenye ndege, choo kidogo na sehemu nyingine ya kujiweka safi. Mashabiki wa West Ham United waliripotiwa kulishambulia kwa mawe basi hilo na kusababisha hasara ya Pauni 1,200. Hiyo ilikuwa mwaka 2016 huko Upton Park.