Ukimchukulia poa ni lazima atakuumiza tu unaambiwa

IKIWA ni miezi minne tu tangu ametua nchini na kubeba mikoba ya kuinoa Simba iliyoachwa na Joseph Omog, Mfaransa Pierre Lechantre anatabasamu tu kwa furaha.

Ndio! Ameipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao makocha waliomtangulia na mabosi wa Wekundu wa Msimbazi waliosotea kwa miaka sita bila mafanikio. Kwake limekuwa jambo linalowezekana na sasa kauli za shombo na kejeli zimehamia upande wa pili kule Jangwani, ambako kuna hali tete kwelikweli kwa sasa.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Lechantre, ambaye ameeleza mambo mengi ambayo amepanga kuyafanya akiwa na Simba msimu ujao.

KIKOSI CHA MZUKA

Mfaransa huyu hafichi kwamba, ametua Simba na kukuta kikosi bora japo kilikuwa na mapungufu machache katika baadhi ya idara ambayo haikuwa kazi ngumu kwake kuyarekebisha.

“Simba ni timu nzuri na ni timu kubwa kwa sababu imecheza na timu bora na imefanikiwa kuibuka na ushindi. Imecheza na Azam FC ikashinda kisha Yanga na kufanya vile vile hivyo, ni timu bora zaidi,” anasema Lechantre.

Hata hivyo, Lechantre amezungumzia ishu ya viwanja ambavyo vimekuwa vikitumika kwa michezo ya Ligi Kuu Bara, ambapo amesema vingi hasa vya mikoani ni tatizo kubwa kwa wachezaji hivyo, kuwafanya washindwe kucheza soka tamu.

Amesema wachezaji wamekuwa wakionyesha kutulia uwanjani na kucheza soka la kuvutia wanapokuwa Uwanja wa Taifa ama Uhuru, lakini kwingine ni majanga.

“Kuna viwanja huko mikoani huwezi kucheza pasi fupi fupi, ni vibovu sana na hili ni changamoto kubwa katika ukuaji wa soka,” anasema.

VIPI Okwi, Bocco

Kama kuna kitu kinachompagawisha Lechante basi ni kuona John Bocco na Emmanuel Okwi wakisimama mbele ya lango la adui. Hapo anakuwa na uhakika wa mabao tena ya kutosha tu na hilo, limemfanya kuwapa umuhimu mkubwa mastaa wake hao. “Nikimuona Okwi na Bocco akili yangu inatulia kabisa, ila wanapokosekana huwa tatizo kubwa. Unajua Simba kuna washambuliaji wawili tu na wasipokuwa fiti kwa asilimia 100 basi kikosi kinayumba,” anasema kocha huyo ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi.

Mchezaji bora wake

“Shomari Kapombe ni mchezaji bora zaidi katika kikosi cha Simba kutokana na kuweza kuelewa vizuri kile ninachokifundisha.

“Tatizo kubwa la wachezaji wa Simba wana uvivu na wanashindwa kunielewa haraka nataka kitu gani. Naweza kuwafundisha leo lakini kesho tu wamesahau hivyo nalazimika kurudia,” anasema.

Pia, anawataja Aishi Manula, Okwi, Jonas Mkude, Bocco na Erasto Nyoni kuwa ni wachezaji waliojitoa kwa hali na mali katika kufanikisha ubingwa wa Simba msimu huu.

Mechi ngumu

Lechantre anasema michezo yake migumu kwa upande wake ilikuwa ugenini dhidi ya Mbeya City , Njombe Mji, Mwadui FC, Mtibwa Sugar, Lipuli na Singida United na sababu kubwa ikikuwa ni hali ya viwanja katika eneo la kuchezea. “Napenda kutumia soka la kushambulia kwa kupasiania pasi za chini hivyo, nilishangazwa na viwanja ambavyo tulicheza. Havikuwa vizuri ingawa hatukupoteza lakini hatukuwa na kiwango kizuri,” anasema.

“Kama ulikuwa unaona wachezaji walikuwa wanapasiana, lakini mpira unadunda jambo ambalo si rafiki na tulilazimika muda mwingi kutumia pasi ndefu za juu ambazo sio nzuri sana kwetu.”

Mechi za Kimataifa zamzingua

“Mechi ya kwanza na Al Masry tulicheza vizuri na tulikuwa na malengo mawili: Tucheze kwa kujilinda na kushambulia kwa haraka jambo ambalo tulifanikiwa, lakini tulifanya makosa kwa kuwaruhusu wapinzani kupata magoli.

“Katika mchezo wa marudiano tulipanga kuzuia dakika 70 na tuliweza lakini zile 20 zilizobaki ambazo tulipanga kushambulia kwa nguvu tulishindwa kuzitumia na ndio sababu hatukufunga bao,” alieleza Lechantre.

VIPI MSIMU UJAO

Kina shabiki wa Simba ana matarajio makubwa ya kwamba, kikosi chao kitatisha zaidi msimu ujao, lakini huko kwa Lechantre kuko hivi.

“Nina mipango kama miwili kwa ajili ya msimu ujao kulingana na mashindano ambayo tutashiriki. Inabidi kufanya usajili wa viwango vya kupambana na TP Mazembe, Al Ahly, Zamaleck na nyingine nyingi.

“Pia, tutaangalia bajeti halisi ambayo tutakuwa nayo katika kufanya usajili kwani, wachezaji bora wote wana gharama kubwa dunia nzima. Sasa itategemea na mabosi zangu watasemaje,” anasema Lechantre na kuiongezea kuwa anasubiri majibu ya bilionea wa Simba, Mohamed Dewji ‘MO’.