Uhuni

Muktasari:

Bao la staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo dhidi ya Juventus limepigwa chini na badala yake bao la Mohamed Salah wa Liverpool dhidi ya Manchester City limechaguliwa kuwa bao bora la robo fainali Ligi ya mabigwa msimu huu.

MADRID HISPANIA

LIVERPOOL itakuwa imefanya uhuni sehemu fulani hivi mitandaoni. Haiwezekani.

Bao la staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo dhidi ya Juventus limepigwa chini na badala yake bao la Mohamed Salah wa Liverpool dhidi ya Manchester City limechaguliwa kuwa bao bora la robo fainali Ligi ya mabigwa msimu huu.

Ronaldo alifunga bao ambalo liliishangaza dunia katika pambano la kwanza la robo fainali dhidi ya Juventus jijini Turin na kuwaacha mashabiki wakiwa midomo wazi huku likiwa moja kati ya mabao bora katika msimu huu na katika historia ya michuano hiyo.

Mashabiki wengi waliamini bao la Ronaldo lilikuwa bora zaidi katika msimu huu lakini wameachwa midomo wazi baada ya bao hilo kushika nafasi ya pili nyuma ya bao la Salah ambaye alifunga kwa kuubetua mpira juu ya kipa Ederson wa Man City katika pambano la marudiano Etihad.

Bao la Salah lilithibitisha kupita kwa Liverpool katika hatua ya robo fainali na kutinga hatua ya nusu fainali na sasa itapambana na Roma ya Italia.

Bao hilo lilipata asilimia 39 ya kura zote mbele ya bao la Ronaldo ambalo lilipata asilimia 30.

Katika mchuano huo, Liverpool iliingiza mabao mawili na bao la staa wake mwingine, Alex Oxlade-Chamberlain ambaye alinunuliwa kutoka Arsenal mwanzoni mwa msimu lilishika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 14 ya kura zote.

Chamberlain alifunga bao hilo katika pambano la kwanza lililochezwa Anfield na alifunga kwa shuti kali akiwa nje ya boksi akimtungua kipa Ederson ambaye alichupa bila ya mafanikio.

Kinachoshangaza ni bao la Salah halijachaguliwa na mashabiki wa Merseyside peke yao na badala yake Uefa imedai mashabiki kutoka pande mbalimbali za dunia walilipigia kura bao hilo na hivyo kumpa ushindi Salah.

Mastaa wote watatu waliopigiwa kura katika mchuano huo wana nafasi ya kufunga bao bora la hatua ya nusu fainali. Wakati Ronaldo ana mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Bayern Munich, Salah na Chamberlaini nao watakuwa na mechi mbili dhidi ya Roma katika hatua hiyo.

Licha ya kuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu ya England na michuano ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya, Salah ana kazi ngumu ya kumpiku Ronaldo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na staa huyo wa Ureno ana mabao 15 mpaka sasa wakati Salah ana mabao manane tu.

Salah amekuwa na wakati mzuri msimu huu na mpaka sasa amefunga mabao 30 katika Ligi Kuu England na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Bara la Afrika kufunga mabao hayo ndani ya msimu mmoja.

Vile vile amefikisha mabao 40 katika michuano mbalimbali na jana alitajwa kuwa mchezaji pekee wa Liverpool kuingia katika kikosi cha mwaka cha msimu huu ambapo Manchester City ilitoa wachezaji watano, Tottenham ikitoa wachezaji watatu huku Liverpool na Manchester United zikitoa mchezaji mmoja mmoja.

Salah pia anatazamiwa kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa msimu huu mbele ya staa wa Manchester City, Kevin de Bruyne kutokana na wachunguzi wa mambo kuwapa kipaumbele mastaa hao wawili waliong’ara zaidi msimu huu.

Tayari staa wa zamani wa England, Alan Shearer pamoja na De Bruyne mwenyewe wamekiri staa huyo anastahili kupewa tuzo ya kuwa Mwanasoka Bora wa England msimu huu baada ya kufanya mambo makubwa kwenye michuano yote anayoshiriki.