USIBISHE: Haya yatatokea Kombe la Kagame

ZIMEBAKI siku kama tano kabla ya michuano ya Kombe la Kagame 2018 kutimua vumbi nchini ikiwa ni miaka miwili tangu ulipochezwa mchezo wa fainali za mwisho mwaka 2015 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika fainali hiyo iliyopigwa Agosti 2, Azam ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wakenya Gor Mahia na kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yake na kuwa timu ya tatu ya Tanzania kutwaa kombe hilo tangu mwaka 1974.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeyarejesha tena mashindano hayo jijini Dar es Salaam na yataanza kuchezwa Juni 29 na kufikia tamati Julai 13 ikishirikisha klabu 12 zikiwano nne za Tanzania.

Watetezi Azam, Mabingwa wa Kihistoria, Simba na Singida United iliyochukua nafasi ya Yanga waliojitoa pamoja na JKU ya Zanzibar ndio watakaopeperusha bendera ya Tanzania katika michuano hiyo iliyodhaminiwa na Azam TV.

Mwanaspoti inakuletea baadhi ya mambo yanayotarajiwa kutokea kwenye michuano ya mwaka huu ambayo ni ya 41 tangu kuasisiwa kwake katika mfumo wa sasa mwaka 1974 na inayotimiza miaka 16 tangu Rais wa Rwanda, Paul Kagame aanze kuipiga tafu.

MICHUANO KUDORORA

Kama kuna kitu ambacho, Cecafa imechemsha ni kuiweka michuano hii sambamba na fainali za Kombe la Dunia inayoendelea nchini Russia.

Tarajio la uongozi wa baraza hilo kupiga pesa michuano ikifanyika jijini Dar es Salaam huenda ikawa kwao, kwani kuna uwezekano mkubwa Kagame Cup 2018 ikadorora.

Hii ni kwa sababu mashabiki wengi watakuwa bize kufuatilia fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea ambapo mechi za makundi zinatarajiwa kumalizika siku moja kabla ya kipyenga cha michuano hiyo ya Kagame.

Licha ya Katibu Mkuu wa Cecafa. Nicholas Musonye kukaririwa akisema walipanga michuano hiyo katika kipindi hiki kwa kuamini haitaathirika, lakini ukweli watarajie kula za uso kwa vile utamu wa fainali za dunia ndio utakuwa umeingia mahali pake.

Timu 16 zitakazofuzu makundi zitaanza kazi ya kulisaka taji hilo linaloshikiliwa na Ujerumani, hivyo ni vigumu mashabiki kukomalia fainali hizo za Kagame badala ya kutaja kujua ni nchi zipi zitacheza hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali yenyewe.

Mbali na fainali hizo za dunia, lakini pia kujitoa kwa Yanga kumepunguza utamu wa Kagame, kwani uwepo wa mabingwa hao mara tano sambamba na Simba na Azam

kungeongeza hamasa na amshaamsha za utani wa jadi. Ngoja tuone itakavyokuwa.

SIMBA ITAFUTA UKAME

Simba inashiriki michuano ya mwaka huu kwa mwavuli wa timu mwenyeji, lakini kwa namna kikosi chao kilivyo na moto ni wazi watafuta ukame wa muda mrefu wa taji la michuano hiyo.

Mara ya mwisho kwa Simba kubeba taji la Kagame lililoifanya iwe kinara ikitwaa mara sita, ilikuwa miaka 16 iliyopita wakati Rais Kagame alijitosa kuidhamini michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Fainali hizo za mwaka 2002 zilifanyika katika ardhi ya Tanzania, lakini upande wa Zanzibar kwa Simba kuikanyaga Prince Louis ya Burundi kwa bao 1-0 na tangu hapo imekuwa ikilisikia tu taji hilo redioni.

Hata hivyo, msimu huu ni wa Msimbazi kama wataamua kuikomalia michuano hiyo na hasa ikizingatiwa inafanyika jijini Dar es Salaam na huku wakitoka kubeba taji la Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

Ikiwa na wachezaji wenye kiu ya mafanikio na vijana wanaotaka kuweka rekodi katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu kwa Afrika Mashariki na Kati, Simba ina kila sababu ya kubeba taji hasa ikizingatiwa kuwa, watani zao Yanga wameingia mitini.

Hii ni michuano ya kina Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Adam Salamba na wengine wasiopata nafasi ndani ya Simba kuonyesha vipaji vyao baada ya kuchemsha kwenye fainali za SportPesa Super Cup 2018 kule Nakuru, nchini Kenya hivi karibuni.

AZAM WATETEZI

Wakati Simba ikipiga hesabu na kupewa chapuo la kulibeba taji hilo kwa mara ya saba, kazi watakuwa nayo mbele ya Azam ambao ni watetezi.

Azam iliyoanza Ligi Kuu ya msimu uliopita kwa kusuasua na hasa baada ya kuondokewa na nyota wake kadhaa waandamizi, ilionyesha wapo moto mwishoni mwa msimu na kumaliza nyuma ya Simba na mbele ya watetezi Yanga walioyumba vibaya.

Kikosi cha Azam kimeimarishwa zaidi mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita kwa kuongezwa majembe kadhaa mapya akiwamo beki Mganda, Nicholas Wadada,

Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu na kumrejesha nyumbani, Mudathir Yahya kunaifanya Azam iwe moto zaidi na kama ikiamua kukaza buti basi taji la Kagame litawahusu tena kwa mara ya pili mfululizo na kurejea ilichokifanya Simba mwaka 1991 na 1992 kabla ya Yanga kujibu mapigo 2011 na 2012.

Chini ya Kocha Hans Pluijm na wasaidizi wake, Idd Nassoro ‘Cheche’ na Juma Mwambusi Azam inatarajiwa kuwakimbiza wapinzani wao kama ilivyofanya fainali za

mwisho walipomaliza michuano hiyo bila kupoteza mchezo wala kuruhusu bao lolote.

Hata hivyo uwepo wa Simba kunaweza kuwatibua kwa sababu mziki wa Vijana wa Wekundu wa Msimbazi sio mchezo.

SINGIDA UNITED KUTETEMESHA

Waliosema kufa kufaana hawakukosea, kwani kujitoa kwa Yanga kumetoa neema kwa Singida United waliopewa nafasi ya kushiriki sambamba na APR ya Rwanda

waliochukua nafasi ya St George ya Ethiopia waliochomoa pia kushiriki mwaka huu.

Washindi hao wa tatu wa SportPesa Super Cup, wanatarajiwa kuleta upinzani katika michuano hiyo wanayoicheza kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo mwaka 2000.

Chini ya Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyeitwa timu akimpokea Pluijm amekuwa akisuka kikosi chake kwa kuwajaribu nyota wapya waliosajiliwa hivi karibuni akiwamo, Eliuter Mpepo, George ‘Tibar’ John na wengine ili kunoa makali kabla ya Kagame.

Kwa namna timu hii ilivyoonyesha upinzani mkali katika Ligi Kuu kwenye msimu wao wa kwanza na kumaliza nafasi ya tano na kufika fainali ya Kombe la FA ikikwama mbele ya Mtibwa Sugar waliobeba ndoo na kile ilichoenda kukifanya Kenya ni wazi, haitakuwa timu ya kubezwa.

RAYON, APR KAZI IPO

Tayari kuna wasiwasi wa Gor Mahia kutuma kikosi kamili katika fainali hizo za Kagame. Kama Wakenya hao wangekuja wangeweza kuzipeleka puta timu za Tanzania a washiriki wengine, lakini utamu utakuwa kwa APR na Rayon Sports za Rwanda ambazo ni wapinzani katika ligi ya kwao.

Kushiriki kwao katikia fainali hizo kwa pamoja kunaongeza udambwidambwi wa michuano ya mwaka huu, japo uwepo wa Kombe la Dunia unaweza kuwatibulia.

Mashabiki walitarajia kushuhudia mechi ya watani mapema kama Yanga ingesalia kundini, lakini baada ya kuingia mitini kwa sasa inasubiriwa kuonwa kama wapinzani hao wa Kinyarwanda zitakutana baada ya kuvuka makundi ili kupata burudani.

MFUNGAJI BORA MGENI

Kama ilivyokuwa kwenye fainali zilizopita zilizofanyika Tanzania na Mkenya Michael Olunga aliyekuwa akiichezea Gor Mahia kubeba Kiatu cha Dhahabu inatarajiwa hata katika fainali za mwaka huu Mfungaji Bora anaweza kuwa nyota wa kigeni.

Haijalishi atakuwa akizichezea timu za Tanzania ama za wageni, kiatu hicho kinawahusu wageni kutokana na umakini wao katika kutupia kambani wanapokuwa uwanjani kwani katika fainali za 2015, Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast aliyekuwa Azam alishika nafasi ya pili sambamba na Osman Bilal Salaheldin wa Al Merreikh waliofunga kila mmoja mabao manne, moja pungufu na aliyokuwa nayo Olunga aliyepo Hispania.

Katika michuano ya SportPesa iliyochezwa Kenya, nyota wa Tanzania walichemsha kwa kushindwa kufunga mabao wakiachwa mbali na wachezaji wa klabu za Kenya.

Meddie Kagere Mchezaji wa Rwanda mwenye asili ya Uganda alimaliza kama kinara kwa mara ya pili mfululizo katika michuano hiyo, kuonyesha wageni walivyo makini.

Hata katika fainali hizo za Kagame sio ajabu kuona tuzo hiyo ikienda tena kwa wageni, huku Wazawa wakiambulia tuzo nyingine ikiwamo wa Kipa Bora

AIBU YA JKU, KATOR, DAKADAHA

Kama ilivyo kwa miaka yote ya michuano hiyo na ushiriki wa timu za Zanzibar, Somalia, Djibout na hata Sudan Kusini waliongia hivi karibuni, zinatarajiwa kuendelea kuwa vibonde na kugeuzwa jamvi la wageni katika michuano hiyo.

Timu za Kator itakayoanza michuano hiyo kuvaana na Azam haitakuwa salama katika Kundi A sambamba na JKU ya Zanzibar, huku Dakadaha ya Somalia iliyopo kundi moja na Simba, Singida United na APR watakuwa na kazi kuvuka salama kundini kama ambayo Ports ya Djibout inavyokuwa na kibarua kigumu katika Kundi B lenye Rayons Sports, Gor Mahia ya kenya na Lydia Ludic ya Burundi ambao wapo vizuri mno.

Hata hivyo kwa kuwa soka ni mchezo wa maajabu, tusubiri tu tuone hali itakavyokuwa katika Kombe la Kagame la mwaka huu, kujua nani atakayecheka ama kulia Julai 13.

MAKUNDI

Kundi A

Azam FC-Tanzania

Kator FC- Sudan Kusini

JKU FC-Zanzibar

Vipers- Uganda

Kundi B

Rayon Sports- Rwanda

Gor Mahia- Kenya

Lydia Ludic- Burundi

Ports- Djibout

Kundi C

Simba- Tanzania

Singida Utd-Tanzania

APR- Rwanda

Dakadaha-Somalia