Jogoo yaipa jeuri UDSM Insider RBA

Muktasari:

Timu ya Jogoo imefungwa pointi 73-70 katika mchezo huo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Bandari jijini Da es Salaam.

KOCHA wa UDSM Insider Mohamed Mgweno  amesema ushindi dhidi ya Jogoo umewaongezea kasi ya kupata matokeo mazuri katika mashindano ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA).

Timu ya Jogoo imefungwa pointi 73-70 katika mchezo huo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Bandari jijini Da es Salaam.

Amesema timu hiyo ilianza ligi kwa kufungwa kutokana na ugeni, lakini ushindi dhidi ya Jogoo umeongeza morali ya wachezaji kufanya vizuri katika mechi zao zijazo.

Kocha wa Jogoo Kabiola Shomari amedai wachezaji wake walikosa umakini na kuruhusu UDSM Insider kuvuna pointi nyingi katika robo nne za mwisho.

Hata hivyo, kujiamini kwa Jogoo kulichangia timu hiyo kupoteza mchezo huo licha ya kucheza kwa kiwango bora.

Robo ya kwanza Jogoo iliongoza kwa pointi 25-15, robo ya pili UDSM Insider pointi 16-11. Robo ya tatu Jogoo ilivuna pointi 18-16 kabla ya kuzidiwa ujanja katika robo ya nne kwa pointi 26-16.

UDSM Insider inashika nafasi ya 13 kati ya timu 16 zinazoshiriki mashindano hayo kwa wanaume.

Timu kongwe ya Oilers inaongoza ligi baada ya kupata pointi 22 ikifuatiwa na Savio yenye pointi 19 katika mechi 11 ambazo kila moja ilicheza.