UBABE TU:Pep arithi kikosi cha Kocha Jupp Heynckes, atamba

Muktasari:

“Ni kocha ambaye anakubalika kwenye timu na kwa kuzingatia rekodi yake Barca anakuwa na aina ya mamlaka ambayo inawahamasisha wachezaji kuwa tayari kujifunza,” anasema Grill.

TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau aliendelea kuzungumza na watu mbalimbali wanaomjua Kocha Pep Guardiola akiwamo Alexis Menuge, ripota wa gazeti la L’Equippe la Ufaransa na Roman Grill wakala wa wachezaji kuhusu utendaji kazi wa kocha huyo. Sasa endelea…

“Ni kocha ambaye anakubalika kwenye timu na kwa kuzingatia rekodi yake Barca anakuwa na aina ya mamlaka ambayo inawahamasisha wachezaji kuwa tayari kujifunza,” anasema Grill.

Mbali na kufanya kazi kwa karibu na Lahm, Grill pia amewahi kuichezea timu ya pili ya Bayern, na amewahi kuwa kocha wa timu ya vijana ya klabu hiyo.

Hakukuwa na shaka katika fikra zake kuhusu sababu hasa ya timu kuwa katika ubora, “Timu ilihitaji mtu kama Pep na kwa hakika sioni kocha mwingine yeyote anayeweza kufanya alichofanya hapa, mwaka jana Bayern walikuwa na kikosi bora katika historia yao yote.

“Kama kikosi hicho kilitengenezwa kwa bahati tu au mipango makini ya timu ya utawala iliyohusisha mbinu za kiuchezaji lakini kilicho wazi, kuna mkakati na mbinu za kiufundi zilizofanywa na Kocha Jupp Heynckes.

“Heynckes alitumia kukubalika kwake na nguvu yake ya kiutawala akiwa kocha mwenye heshima zake na mzoefu kuongoza watu wake lakini wachezaji walikuwa wakija na mbinu zao wenyewe uwanjani na wasingeweza kuendelea nazo kwa mwaka mmoja uliofuata hasa baada ya kuwa tayari walishashinda kila kitu.

“Walihitaji kuchangamshwa na kocha mwenye mawazo mapya, kocha ambaye ana mipango na ana utaratibu wa kuifanyia kazi kila siku, hakuna kocha mwingine duniani ambaye angeweza kuwapa mambo haya, ni Pep pekee.

“Timu imepitia hatua za kipekee za mabadiliko na sijawahi kuiona Bayern ikicheza kwa kiwango cha juu na kasi ya aina hii, mechi ya mjini Manchester dhidi ya Man City ilikuwa ya kipekee, iliyopendeza kuangalia, Pep kwa wakati wote anajua nini anachotaka.

“Ni mtu ambaye anataka kuwasaidia wachezaji wake, anataka kufanya nao kazi si kwenda kinyume nao, pia yuko wazi kwa kile anachotaka, anaangalia nini malengo yake.”

Baada ya mazungumzo haya nilikutana na Daniel Rathjen, Mjerumani mwandishi wa Eurosport ambaye amekuwa akiifuatilia Bayern kwa karibu katika kipindi chote cha msimu.

“Majira ya baridi ilikuwa kipindi cha aina yake cha mabadiliko kwa Pep na Bayern, alikuja hapa majira ya kiangazi akiwa na falsafa zake na mawazo yake mapya lakini hiyo bado ilikuwa ni timu ya Heynckes, ungeweza kulibaini hilo kwa wachezaji, kwa mabosi na hata kwa Pep mwenyewe.

“Ungeweza kuliona hilo kwa namna ambavyo walikuwa wakicheza na ilikuwa ni changamoto kubwa ya kubadili hali hii, ilikuwa ni jambo ambalo lingechukua muda nafikiri kule Marrakesh kulikuwa kila kitu katika kubadili mambo, baada ya kubeba taji la klabu la dunia, kwa mara nyingine Pep alimshukuru Heynckes.

“Alisema wakati akimshukuru, asante Jupp (Heynckes) kwa kutupa nafasi ya kubeba taji hili.” Lakini hilo lilikuwa ni tukio la kupita, ni taji la mwisho kubebwa na timu ya zamani.

“Wakiwa Qatar, mara baada ya mapumziko ya majira ya baridi, hapo ndipo zama za Pep zilipoanza, wachezaji kina Robben, Schweinsteiger, Lahm na Ribery walielewa bado walikuwa na nafasi ya kushinda mataji zaidi na hapo ilikuwa rahisi kwa Pep kuvuna matunda ya alichokipanda.

“Wiki ya kuelekea Februari ilitumika kwa ajili ya kujuana, kuweka utaratibu wa kila siku na kukabiliana na majanga ya rundo la wachezaji waliokuwa majeruhi ambalo lilikuwa likiwaandama lakini pamoja na hali hiyo bado Bayern ilifanikiwa kuitawala ligi.