Tuna kila sababu ya kuwahurumia Wadachi

Muktasari:

Nilitumia wiki hii kuendelea kuomboleza msiba ambao unaendelea kuikabili Uholanzi katika soka. Inasikitisha na inatia simanzi. Soka la Uholanzi lipo pabaya na linakatisha tamaa. Unashindwa kuamini kama ni taifa lile lilotesa kisoka.

NI wikiendi ya mechi za kimataifa. Wikiendi ambayo binafsi siipendi. Inapoteza muda tu na inakata utamu wa ligi mbalimbali zinazoendelea duniani kote hasa ligi yetu pendwa ya England ambayo imetuteka kwa miaka nenda rudi.

Nilitumia wiki hii kuendelea kuomboleza msiba ambao unaendelea kuikabili Uholanzi katika soka. Inasikitisha na inatia simanzi. Soka la Uholanzi lipo pabaya na linakatisha tamaa. Unashindwa kuamini kama ni taifa lile lilotesa kisoka.

Nilikuwa nakagua kikosi chao majuzi wakati Kocha Ronald Koeman alipokiita tena. Mchezaji pekee ambaye anasimama juu ya wengine kwa kiasi kikubwa ni beki, Virgil van Dijik. Taifa lina mchezaji ghali kuliko wote halafu ni beki.

Uholanzi ambayo tuliifahamu sisi ilikuwa ina mastaa wengi wa eneo la ushambuliaji na kiungo. Sihitaji kukumbusha sana enzi za kina Patrick Kluivert au Dennis Bergkamp. Katika eneo la kiungo sihitaji kukumbusha sana zama za kina Edgar Davids na wengineo

Leo staa wa Uholanzi ni beki. Leo mchezaji ghali wa Uholanzi ni beki. Katika kikosi chao kuna watoto wadogo na baadhi ya watu wazima ambao hawajawahi kuuzwa hata kwa Pauni 30 milioni.

Mpaka leo Ryan Babel ambaye Liverpool imeshamsahau kumbe kwao ni miongoni mwa mastaa wa timu ya taifa.