Tshishimbi amkata straika Yanga

Muktasari:

  • Hivyo uwepo wa Tshishimbi na Fiston umesababisha kukatwa kwa mchezaji huyo mpya

STAA wa Yanga, Papy Tshishimbi, amependekeza jina la straika matata kutoka moja ya klabu za DR Congo, lakini kocha George Lwandamina, amewaambia viongozi hata kama straika huyo ni mzuri kiasi gani, Wakongomani wametosha Jangwani.

Yanga wamekata jina la mchezaji huyo baada ya kuamua kumalizana na beki mpya, Fiston Kayembe ambaye pia ni pendekezo la Tshishimbi. Hivyo uwepo wa Tshishimbi na Fiston umesababisha kukatwa kwa mchezaji huyo mpya, ambaye viongozi walipanga kumalizana naye haraka ili atue wambwage Donald Ngoma ambaye amekuwa butu. Lakini, wakabaini Wacongo watakuwa wengi na inaweza kuleta shida kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa miaka ya 2000 iliposajili watatu chini ya Kocha Mkongomani, Papa Polycarp Bonghanya.

Walichoambiwa viongozi na makocha ni  kwamba, Kayembe na Papy Tshishimbi ambaye ni kiungo wanatosha, kumsajili tena mshambuliaji kutoka Congo itakuwa imefanya timu hiyo kuwa na raia watatu kutoka nchi moja jambo ambalo linaweza kuleta shida. Mwanaspoti linafahamu kuwa tayari Yanga ilikuwa katika hatua nzuri kumalizana na straika mmoja wa maana kutoka DR Congo ikiwa ni mapendekezo ya Tshishimbi. Mmoja wa vigogo wenye ushawishi kwenye kamati ya usajili wa Yanga, amesema wameamua kuzingatia ushauri huo ili kuepusha shari na sasa wameelekeza nguvu kwenye nchi nyingine za Afrika.

“Ni kweli tumetoa ushauri huo, unajua wachezaji wengi wa Kiafrika weledi wao umekuwa mdogo hasa kunapotokea mambo tofauti, sasa unapokuwa na wachezaji zaidi ya wawili kutoka katika nchi moja au hata timu moja, wanaweza kuwapa shida katika uangalizi wake, lakini ukiacha hilo nimekuwa sina utaratibu wa kusajili wachezaji wawili au zaidi ya wawili kutoka sehemu moja,” alisema Lwandamina.

ILIWAHI KUTOKEA

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 Yanga ilikumbana na sekeseke la wachezaji kutoka DR Congo. Ilikuwa na mastraika wawili, Pitchou Kongo na Patrick Katalay pamoja na beki Alou Kiwanuka.

Wachezaji hao licha ya kufanya vizuri uwanjani na kuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza, walikuwa wakiisumbua klabu hiyo kwa vile mambo mengi walikuwa wakishauriana na kufanya kwa pamoja ikiwamo safari za kwao, kuchagua mechi za kucheza pamoja na kushinikiza masilahi binafsi.

Rekodi zinaonyesha kwamba kuna wakati walikuwa wakienda kwao na kuchelewa kurudi kwa makusudi na kulazimika Yanga kupanda ndege kuwafuata na walikuwa wakisingizia majeruhi na matatizo ya kifamilia mara nyingi mpaka Yanga ilipokuja kuwabwaga kwa nyakati tofauti pamoja na kocha Bonghanya.

Bonghanya alitimuliwa Yanga na mashabiki ambao walimzuia kuingia Uwanja wa Kaunda kufundisha timu kwa kufunga milango huku wakimuonyesha alama X kwa mikono na kutamka ‘Closed’ wakimaanisha pamefungwa huku wachezaji wakiendelea kupasha kivyao.

NANE INGEPENDEZA

OBREY Chirwa ameendelea kuthibitisha kwamba ndiye staa wa Yanga kwa sasa baada ya jana Jumapili kufunga mabao matatu ‘hatrick’ katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Mbeya City lakini mashabiki wa Jangwani wakawa wanatamba kwamba ‘Nane ingependeza zaidi’ ili kufunika rekodi ya Simba iliyowahi kumpiga Ruvu Shooting mabao 7-0.

Chirwa alifungua akaunti yake ya mabao dakika ya 19 akiunganisha pasi ya Pius Buswita aliyetumia vizuri uzembe wa walinzi wa City waliodhani kwamba mpira umetoka.

Mchezaji huyo bora wa Ligi Kuu kwa mwezi Oktoba alifunga mabao mengine mawili katika dakika ya 49 kwa mkwaju wa penalti na dakika ya 19 kwa mpira wa kuchopu akiunganisha pasi ya Ibrahim Ajibu.

Chirwa amefikisha mabao sita Ligi Kuu na kuwa mchezaji wa pili kufunga hatrick msimu huu, baada ya ile ya Emmanuel Okwi wa Simba.

Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na Emmanuel Martins katika dakika ya 22 akiunganisha pasi ya Raphael Daud na katika dakika ya 80 akimalizia pasi nzuri ya beki wa kushoto, Gadiel Michael.

Matokeo hayo yanaiacha Yanga katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 20. Simba ndiyo vinara wakiwa na pointi 22 sawa na Azam iliyopo katika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mechi nyingine jana Jumapili, bao pekee la Aggrey Morris kwa mkwaju wa penalti lilitosha kuipa Azam ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Njombe Mji wakati Kagera Sugar ilifufukia kwa ndugu zao, Mtibwa Sugar kwa ushindi wa 1-0 pia.