Try Again afichua mazito ya MO Simba

Muktasari:

Si Yanga wala timu zingine ambazo MO anataka ziwe wapinzani wa Simba, bali kuwa timu ya kushindana na vigogo wengine Afrika

Dar es Salaam. MASHABIKI wa Simba wanafikiria kuhusu kikosi cha kutetea taji la Ligi Kuu Bara, lakini kumbe akili ya bilionea wao namba moja Mohamed Dewji (MO) inawaza mbali zaidi.
Tangu wakati akitangaza kumwaga pesa ndefu kwa ajili ya kuwekeza na kueleza adhma ya kubadili muundo na utendaji ndani ya Simba, Mo alionyesha kuwa kuna kitu cha ziada anakihitaji.
Tayari Simba imeanza kuonyesha mwelekeo tofauti kabisa na klabu zingine za Ligi Kuu Bara na hata Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, jambo ambalo limewapa mashabiki wake matumaini mapya kabisa.
Hata hivyo, wakati mashabiki wakidhani kila kitu kimefika mwisho ama kuridhika na kinachoendelea kwa sasa, imefichuka kuwa MO bado hajaridhika kabisa akitaka kuifanya Simba kuwa klabu isiyowaza wapinzani uwanjani.
Si Yanga wala timu zingine ambazo MO anataka ziwe wapinzani wa Simba, bali kuwa timu ya kushindana na vigogo wengine Afrika kisha hapa Bongo iwe tishio pekee kama ilivyo Bayern Munich kule Bundesliga ambapo, kila msimu imekuwa ikibeba tu mataji.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' alifichua kuwa MO hana mpango wa kutengeneza Simba ili kuwa tishio kwenye Ligi Kuu Bara tu, bali kupambana na timu zingine kubwa zaidi Afrika.
Alisema Simba mikakati ya MO ni kuifanya Simba kuwa kwenye ushindani na timu kama TP Mazembe ya DR Congo, ambayo ilipata kucheza na Inter Milan kusaka kombe la Dunia kwa klabu, ambapo kwenye mchezo huo Samuel Eto’o aliwazima ndugu zake wa Afrika kwa kupachika bao matata huku benchi la ufundi la mabingwa hao wa Serie A likiongozwa na kocha wa sasa wa Manchester United, Jose Mourinho.
“Simba inayokuja haitakuwa ile mliyowahi kuiona katika miaka yote huko nyuma, MO anataka Simba yenye kutamba Afrika na nje ya mipaka ya bara hili. Hapa tulipo ni mwanzo tena wa mbali sana katika kusuka klabu ambayo haitakuwa na mpinzani wa kushindana nayo,” alisema Try Again.
Pia, amefichua kuwa MO ameingia Simba kwa ajili ya kuhakikisha anaiwezesha kufikia viwango vya kimataifa na sio kufanya biashara.
Try Again, ambaye ameiongoza Simba kuingia kwenye hatua ya muundo huo mpya na kuiwezesha kubeba ubingwa na kuvunja unyonge kwa Yanga, amesema MO huumia na kujisikia vibaya pindi timu inapofanya vibaya. “Simba inapofanya vibaya uwanjani, MO anakuwa kwenye wakati mgumu kuliko hata mashabiki, ana mapenzi ya dhati na timu yake,” aliongeza.
Kuhusu mafanikio ambayo yameanza kuonekana ndani ya Simba kwa sasa, Try Again amesema kila eneo MO ana mchango wake na kwamba, hata kama yeye akiondoka kwa sasa anaamini Wekundu hao wa Msimbazi watabaki salama chini ya bilionea huyo kijana.
"MO anaipenda Simba, kama kuna mtu anadhani amekuja kufanya biashara huyo hafahamu kabisa, kila anapoamka na kulala anaiwaza Simba tu, mipango na akili yake ni kuifanya kuwa timu kubwa Afrika," alisema.
"Binafsi nimefarijika kwamba hata ninapoondoka kwa sasa Simba itaendelea kuwa moto chini ya MO, iko kwenye mikono salama na itaendelea kujitanua na kufanya makubwa zaidi,”