Top Six kali ya Wenger tangu atue England

Muktasari:

Pointi hizo za Arsenal zimeizidi West Brom inayoburuza mkia msimu huu kwa pointi 32. Kwa maana hiyo, Arsenal ipo karibu na timu inayoshuka daraja kuliko mabingwa wa msimu huu.

LONDON, ENGLAND. CHUKUA msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, Arsenal ipo kwenye nafasi ya sita huko na pointi zake 57, pointi 33 nyuma ya vinara na mabingwa Manchester City. Ni aibu.

Pointi hizo za Arsenal zimeizidi West Brom inayoburuza mkia msimu huu kwa pointi 32. Kwa maana hiyo, Arsenal ipo karibu na timu inayoshuka daraja kuliko mabingwa wa msimu huu. Pengine hilo ndilo lililowafanya mabosi wa Arsenal kufikiria kufanya mabadiliko ya benchi lao la ufundi kwa kumwaambia kocha wao, Arsene Wenger akampumzike tu. Wenger atakusanya mikoba yake na kuachana na Arsenal mwishoni mwa msimu huu baada ya kudumu kwenye kikosi hicho kwa karibu miaka 22, maana alitua kwenye timu hiyo Oktoba 1996.

Hata hivyo, aibu hiyo ni kwa msimu huu tu, lakini ukichukua rekodi za jumla ya mechi zote za Ligi Kuu England zilizochezwa tangu Wenger alipotua kwenye ligi hiyo, Man City hata kwenye Top Six haipo.

Wababe hao wa Etihad, tangu wakati huo, wamecheza mechi 641, wameshinda 310, sare 139, vichapo 192 na wamekusanya pointi 1,069.

Huu hapa msimamo wa Top Six unaoanzia tangu Wenger alipotua kwenye Ligi Kuu England hadi sasa. Hata hivyo, hauhusishi mechi za mwisho walizocheza kwenye ligi hiyo.

6.Everton - mechi 824, pointi 1,149

Kwa msimu wa muda wote tangu Wenger alipoingia kwenye Ligi Kuu England, Everton ndiyo inayoshikilia nafasi ya sita kutokana na kucheza mechi 824 na kukusanya jumla ya pointi 1,149.

Katika mechi hizo, Everton imeshinda 303, imetoka sare 240 na kupoteza mechi 281. Katika kipindi hicho, Everton imepita chini ya makocha wengi tofauti, lakini David Moyes alidumu hapo kwa miaka isiyopungua 10.

5.Tottenham - mechi 824, pointi 1,280

Wenger baada ya kutua tu Arsenal akaambiwa Tottenham Hotspur ndiyo mahasimu wao wakubwa kwenye soka la England. Kutokana na hilo kama itaamriwa kutengenezwa msimamo wa tangu Wenger alipotua kwenye Ligi Kuu England, Spurs itashika nafasi ya tano baada ya kucheza mechi 824 na kukusanya pointi 1,280. Katika mechi hizo imeshinda 359, sare 203 na vipigo 262.

4.Liverpool - mechi 824, pointi 1,463

Wababe wa Anfield, wameanza ubabe siku nyingi tu. Wanashika nafasi ya pili kwa mataji ya ligi huko England. Lakini, kama ingekuwa kutengeneza msimamo wa kuanzia tangu Wenger alipoingia kwenye Ligi Kuu England, Liverpool ingekamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sababu itakuwa inashika namba nne kwa kucheza mechi 824 na kuzoa pointi 1,463. Liverpool imeshinda mechi 418, sare 209 na vichapo 197.

3.Arsenal - mechi 823, pointi 1,618

Hiki ndicho kinachomfanya Arsene Wenger ahesabike kuwa bonge la kocha kwenye Ligi Kuu England kwa sababu hata rekodi za kuanzia tangu alipotua kwenye ligi hiyo, ukitengenezwa msimamo timu yake haitoki nje ya Top Four.

Kwa msimamo wa tangu wakati huo, Arsenal inashika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 1,618 katika mechi 823 ilizocheza na kushinda mechi 473, sare 199 na kupoteza mechi 151.

2.Chelsea - mechi 824, pointi 1,628

Chelsea ni chama jingine ambalo limekuwa likifanya vizuri tangu Ligi Kuu England ilipoanza. Kwa kuanzia tangu alipotua Wenger kwenye ligi hiyo mwaka 1996, Chelsea imecheza mechi 824 na kuvuna pointi 1,628.

Katika mechi hizo ilizocheza imeshinda 480, sare 188 na kupokea vichapo katika mechi 156. Si rekodi mbaya na ndiyo maana kama unatengenezwa msimamo wa kuanzia wakati huo, Chelsea inashika namba mbili.

1.Man United - mechi 824, pointi 1,733

Manchester United rekodi yake kwenye soka la England ni matata sana. Ndiyo timu iliyoshinda mara nyingi katika kila timu iliyowahi kucheza nayo. Jambo hilo ndiyo maana inakuwa juu kwenye soka hilo.

Kwa kutazama rekodi zake kuanzia tangu Wenger alipotua kwenye Ligi Kuu England, Man United imecheza mechi 824 na kuvuna pointi 1,733, hivyo kama ungetengenezwa msimamo tangu wakati huo, yenyewe ingekuwa namba moja baada ya kushinda mechi 521, sare 170 na vichapo 133.