Timu tatu zachanua Ligi Daraja la Kwanza

Muktasari:

  • Timu hizo tatu zimeibuka na ushindi mfululizo kwenye mechi zao mbili za awali za FDL zikiwania kupanda Ligi Kuu msimu ujao, hata hivyo Mingange alisema  ni mapema kuanza kuzitabiri kwa sasa kwa mechi mbili za kwanza.

KASI ya KMC, JKT Ruvu na Dodoma FC zimekuwa tishio katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL)  lakini bado imeonekana kuwa sio tishio mbele ya Kocha wa Mshikamano, Abdul Mingange anayeamini timu hizo bado zina safari ndefu.

Timu hizo tatu zimeibuka na ushindi mfululizo kwenye mechi zao mbili za awali za FDL zikiwania kupanda Ligi Kuu msimu ujao, hata hivyo Mingange alisema  ni mapema kuanza kuzitabiri kwa sasa kwa mechi mbili za kwanza.

"Ni kweli zinafanya vizuri na katika ligi hii jambo la msingi ni kupata pointi tatu muhimu, lakini binafsi naamini ligi hii ni ndefu na kuna idadi kubwa ya mechi zimebakia mbele ya safari kwa kila timu.

Unaweza kukuta timu nyingine zinabadilika na kufanya vizuri zaidi hapo baadaye na zikafanikiwa kupanda. Ni mapema mno kuziona hizo timu zimeshapanda kwa kuangalia matokeo ya mechi mbili," alisema Mingange.

Akitolea mfano wa kundi lake, Mingange alisema sio gumu kama wengi wanavyohisi kwani linajumuisha timu anazozifahamu vizuri.