VIDEO-Simba yapata somo yajipanga upya

Muktasari:

  • Vinara hao wa Ligi Kuu Bara watalazimika kutwaa ubingwa wa ligi ili kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma amesema wamejifunza mambo mengi katika mashindano ya kimataifa msimu huu na sasa wanajipanga upya kwa msimu ujao.

Simba waliondolewa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kulazimisha suluhu na Al Masry ugenini baada ya mchezo wa awali kutoka sare 2-2 Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 6:30 mchana, Djouma alisema wamejifunza ili kujipanga kwa msimu ujao wasikosee tena kama watapata nafasi ya kucheza tena.

"Kwa miaka mingi Simba haikushiriki mashindano ya kimataifa mwaka huu tumepata fulsa hiyo, lakini tumeona umuhimu wa kucheza mashindano haya kwani kuna mengi tumejifunza," alisema Mrundi huyo.

"Tumeona wenzetu wanavyojianda nje na ndani ya uwanja kuelekea katika mechi za kimataifa, hata wanavyocheza wakiwa katika mechi ya ugenini na nyumbani jambo ambalo tunakwenda kulifanyia kazi ili kulitumia msimu ujao kama tutapata tena nafasi," alisema Djuma.

"Katika mashindano ya kimataifa wenzetu huwa wanatumia vizuri muda katika kufanya maandalizi kwa ajili ya mashindano haya na ndio maana ukifuzu katika hatua moja kwenda nyingine unakutana na timu ngumu zaidi tumeyachukua hayo na msimu unaokuja tutakuwa imara zaidi," alisema Djuma.