Tevez amzuia Messi kustaafu

Mshambnuliaji wa zamani wa Argentina, Carlos Tevez,34, amemsihi nahodha wa kikosi cha sasa cha nchi hiyo, Lionel Messi, kuachana na mpango wake wa kutaka kustaafu soka la kimataifa.

Tevez aliyeichezea Argentina mechi 76, amemzuia Messi kustaafu soka la kimataifa, uamuzi alioufikia siku chache baada ya Argentina kutolewa katika fainali za Kombe la Dunia 2018, zilizomalizika wiki iliyopita nchini Russia.

Alisema anafahamu maumivu aliyoyapata Messi na wachezaji wote baada ya Argentina, kutolewa na Ufaransa, katika 16 bora ya fainali hizo, lakini hilo halipaswi kuwa sababu ya kustaafu wakati bado anayo nafasi muhimu ya kuisaidia nchi yake kimataifa.

Tayari aliyekuwa Kocha wa Argentina katika fainali hizo Jorge Sampaoli, ameshajiuzulu kuinoa timu hiyo kutokana na matokeo hayo mabaya, yaliyowaumiza mashabiki na wananchi wote wa Argentina.

Katika fainali hizo Argentina haikuonyesha soka zuri ndio maana hata matokeo yao hayakuwa mazuri, ilianza kwa sare ya bao 1-1 na Iceland ikafungwa 3-0 na Croatia, kabla ya kuifunga Nigeria kwa mabao 2-1 na kutinga 16 bora ambako iling’olewa na Ufaransa kwa kufungwa mabao 4-3.

Messi mshindi mara tano wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Dunia ‘Ballon d'Or’ ambaye ana miaka 31 alikaribia kustaafu mwaka 2016 baada ya Argentina kufungwa na Chile katika mechi ya fainali ya Copa America lakini wengi walimsihi na akabadili uamuzi.

"Bila shaka uamuzi wa Messi kutaka kustaafu soka la kimataifa sio wa busara, hii ni kama askari anayetegemewa akakimbia vitani, kwangu mimi busara ni kwa Messi kubaki na kujaribu nafasi nyingine ya kuisaidia Argentina kushinda ubingwa,” alisema.

Tevez mwenye miaka 34 alisema Messi bado anao uwezo wa kuisaidia nchi yake kutokana na kipaji alichonacho katika soka, hivyo ajipe muda wa kujaribu tena badala ya kukata tamaa.

Makocha kadhaa wametajwa kuwa na nafasi kubwa ya kumrithi Sampaoli, miongoni mwao ni Kocha wa Peru, Ricardo Gareca, Kocha wa zamani wa Argentina, Jose Pekerman ambaye kwa sasa anainoa Colombia, hata hivyo Chama cha soka Argentina (AFA) bado hakijatamka lolote kuhusiana na uteuzi wa Kocha mpya.