Teknolojia ya VAR yaibeba Marseille

Muktasari:

  • VAR ilianza kutumika katika mchezo wa ufunguzi wa msimu uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Orange Velodrome kati ya Marseille dhidi ya Toulouse.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji wa Marseille, Dimitri Payet amekuwa wa kwanza kunufaishwa na matumizi ya teknolojia ya bao ‘VAR’ inayotumika kwa mara ya kwanza katika Ligi kuu Ufaransa msimu huu.

VAR ilianza kutumika katika mchezo wa ufunguzi wa msimu uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Orange Velodrome kati ya Marseille dhidi ya Toulouse.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa West Ham alifunga mabao mawili katika mchezo huo, lakini bao la kwanza alilolifunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 45 lilitokana na uamuzi ya VAR.

Mwamuzi wa mchezo huo Ruddy Buquet aliamuru mpira upigwe kona, lakini waamuzi waliopo kwenye VAR wakaamuru ipigwe penalti kwa madai mpira wa kichwa uliopigwa na Valere Germain ulimgonga mkononi mlinzi Toulouse.

Mchezaji huyo mwenye miaka 31 baadaye aliifungia timu yake bao la pili kwa shuti kali katika dakika ya 62 kabla ya Germain kufunga la tatu dakika ya 89 ma Florent Thauvin kafunga la nne dakika za majeruhi.