Tayari ligi ya malkia yarejea rasmi

Muktasari:

  • Manchester City ni mabingwa watetezi wa ligi hii na klabu nyingine kubwa zilizobaki Manchester United, Liverpool, Arsenal, Chelsea na Tottenham kuanzia leo zitaanza kibarua rasmi za kujaribu kuwavua ubingwa.

MANCHESTER, ENGLAND. Tayari imerudi. Ni ile Ligi inayoacha mashabiki wake wakiwa na machozi, jasho, damu, tabasamu, hasira, vicheko na mshangao. Ligi Kuu England imerudi tena na leo kuna pambano moja kati ya Manchester United na Leicester City pale Old Trafford.

Manchester City ni mabingwa watetezi wa ligi hii na klabu nyingine kubwa zilizobaki Manchester United, Liverpool, Arsenal, Chelsea na Tottenham kuanzia leo zitaanza kibarua rasmi za kujaribu kuwavua ubingwa.

Katika pambano la leo, United wanaingia uwanjani huku kocha, Jose Mourinho akidai kupitia kipindi kigumu cha maandalizi ya msimu mpya tangu awe kocha baada ya timu hiyo kuwa na wakati mgumu wa kuwanasa mastaa ambao waliwahitaji.

Kama vile haitoshi, Mourinho hakufanikiwa kwenda Marekani na baadhi ya mastaa wake ambao nchi zao zilifika mbali katika michuano ya kombe la dunia nchini Marekani kama vile Paul Pogba, Marouane Fellaini, Romelu Lukaku, Jesse Lingard, Marcus Rashford na Ashley Young.

Huenda mastaa hao wasicheze katika pambano la leo na kama watacheza bado hawatakuwa fiti kama ambavyo inatakiwa. Mourinho anatazamiwa kuwatumia zaidi mastaa aliyokwenda nao Marekani ambao hata hivyo hawakuonyesha viwango vizuri.

Mourinho pia aliingia katika bifu na staa wake wa kimataifa wa Ufaransa, Anthony Martial ambaye aliondoka katika kambi ya mazoezi ya Marekani na kurudi kwao Ufaransa kwa ajili ya kushuhudia kuzaliwa kwa mtoto wake wa pili wa kiume.

Martial hakurudi tena Marekani huku Mourinho akidai kwamba alikuwa anamsubiri staa huyo arudi tena kambini na inasemekana kwamba Martial aliwaambia wachezaji wenzake kuwa anataka kuondoka Old Trafford katika dirisha lililofungwa jana usiku.

Kiungo Nemanja Matic hatacheza katika pambano la leo baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo kufuatia maumivu aliyopata akiwa na kikosi cha Serbia katika michuano ya kombe la dunia nchini Russia.

Mabeki wawili wa kulia, mkongwe Antonio Valencia na kinda, Diogo Dalot aliyenunuliwa kutoka Porto katika dirisha hili la uhamisho wote ni majeruhi na kuna uwezekano Mourinho akawatumia ama Victor Lindelof au Eric Bailly kucheza kulia.

Beki wa kimataifa wa Argentina, Marcos Rojo naye ni majeruhi ingawa pia alikuwa akihusishwa kuondoka katika dirisha lililofungwa jana kama ilivyo kwa mlinzi mwingine, Matteo Darmian ambaye naye alikuwa katika hatihati ya kuondoka.

Kwa upande wa Leicester City, kocha Mfaransa wa timu hiyo hakuwa na matatizo mengi katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya kama ilivyo kwa Mourinho lakini alikuwa na hatihati ya kuwakosa mastaa wake wawili, mshambuliaji Jamie Vardy na mlinzi, Harry Maguire.

Hata hivyo, Maguire alikuwa katika hatihati ya kutua United jana kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho huku hadi jana asubuhi Leicester wakiwa wamekataa ofa mbili za United moja ikiwa ya pauni 60 milioni na wanataka kumfanya mlinzi huyo wa England kuwa beki ghali duniani.

Tayari Puel amedai kwamba hakuna mchezaji yeyote kati ya hao ambaye anaweza kuanza lakini kuumia kwa mlinzi, Jonny Evans aliyenunuliwa kutoka West Brom kunaweza kumlazimisha Puel ampange Maguire kama mpaka jana usiku uhamisho wake wa kwenda Old Trafford utakuwa haujakamilika.

Nafasi ya Vardy itazibwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Kelechi Iheanacho ambaye ametamba katika mechi za maandalizi ya msimu mpya akiwa amefunga mabao manne katika mechi tatu za maandalizi.

Staa mpya wa timu hiyo, James Maddison ambaye amenunuliwa kutoka Norwich City naye anaweza kuanza pambano la kesho huku staa mwingine mpya Rachid Ghezzal aliyenunuliwa kutoka Monaco kwa ajili ya kuziba pengo la staa mwenzake wa Algeria, Riyad Mahrez aliyetimkia Manchester City.