Tarimba afunga kazi dili la Yondani

Muktasari:

  • Yondani, ambaye ni nahodha msaidizi wa Yanga, amekuwa akitajwa kutakiwa na Simba, ambao hata hivyo wamekanusha kusaka saini ya beki huyo aliyekuwa kwenye kiwango cha juu msimu uliopita.

MABOSI wa Yanga wako kwenye hatua za mwisho kabisa kumalizana na beki wao, Kelvin Yondani baada ya tishio kwamba, anataka kwenda Simba.
Yondani, ambaye ni nahodha msaidizi wa Yanga, amekuwa akitajwa kutakiwa na Simba, ambao hata hivyo wamekanusha kusaka saini ya beki huyo aliyekuwa kwenye kiwango cha juu msimu uliopita.
Iko hivi. Jana Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Yanga, ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo, Abbas Tarimba alikutana na Yondani ofisini kwake kuzungumzia ishu ya mkataba mpya. Mbali na Yondani, Tarimba pia alikutana na beki Hassan Kessy ambaye naye hajasaini mkataba mpya mpaka sasa. Mabeki hao wote wamegoma kusafiri na timu ambayo iko Nairobi, Kernya kuvaana na Gor Mahia.
Mwanaspoti ambalo liliweka kambi ofisini kwa Tarimba maeneo ya Oysterbay, lilishuhudia Yondani akiingia kuzungumza na kigogo huyo na taarifa zinaeleza kuwa, mambo ni freshi.

Picha zima lilivyokuwa:
Mapema jana asubuhi Mwanaspoti liliingia kazini kwa shughuli nyingine ya kimafia, baada ya kutonywa kuwa Yondani atafika kwa Tarimba kumaliza dili lake.
Haikuwa kazi rahisi kwani timu ya Mwanaspoti ililazimika kuweka kambi jirani na jengo la ofisi zilizopo Kampuni ya SportPesa kwa saa kabla ya Yondani na timu yake kuwasili eneo hilo.
Saa 4:26 asubuhi Yondani akiwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Carina sambamba na Kaka yake Sunday na Crouch, ambapo haraka haraka waliingia kwenye ofisi za Tarimba.
Mazungumzo ya Yondani na Tarimba yalidumu kwa saa moja na nusu, ambapo baada ya kufikia mwafaka beki huyo kwa mara nyingine akiwa mwenye tahadhari aliingia kwenye gari fasta.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa kama sio jioni basi kesho Yondani atakuwa amemwaga wino kweye mkataba wa miaka miwili kubaki Yanga.

Kessy anafuata
Baada ya Tarimba kumalizana na Yondani, ambaye ni nahodha msaidizi jana hiyo hiyo alikuwa akisubiriwa Kessy kwenda kukutana na kigogo huyo ili kumaliza ishu yake.