Tanzanite yafanyiwa fitna mwanzo mwisho Nigeria

Muktasari:

  • Mchezo huo utafanyika leo kwenye Uwanja wa  Ogbemudian uliopo katika mji wa Benin na utaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Nigeria sawa na  saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Timu ya Soka ya Wanawake chini ya miaka 20 ‘Tanzanite' iko kamili kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Nigeria wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Ufaransa mwaka 2019 huku kikosi hicho kikikumbana na fitna za nje ya uwanja.

Mchezo huo utafanyika leo kwenye Uwanja wa  Ogbemudian uliopo katika mji wa Benin na utaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Nigeria sawa na  saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na mwandishi kutoka Nigeria, kocha wa Tanzanite, Sebastian Nkoma alisema wamekuwa na tahadhali kubwa kuelekea mchezo huo kwani tayari wapinzani wao wameshaanza kuwafanyia fitna za nje ya uwanja.

 

"Tumekuwa na tahadhari kubwa tangu tunatoka nyumbani. Timu yao huku haitangazwi sana kwani tangu tumefika mji wa Benin  ndio leo wametangaza kuwa timu yao inacheza. Wako kimya lakini tunajua kuna vitu wanavificha.

 

"Tuko makini kwa hili, tunajua Nigeria ni taifa kubwa kwenye soka hivyo tutacheza kwa tahadhari ili kupata matokeo ambayo yatatusaidia kuwamaliza nyumbani," alisema Nkoma.

 

Aliongeza, "Kwanza tulichelewa kufika huu mji wa Benin ambapo ndipo mechi inafanyika kwa sababu  usafiri  wa kuja huku ni mgumu na yote yalisababihwa na wao ikiwa ni mbinu zao za kushinda nje ya uwanja, kwani walitufanyia fitna za kuchelewa ndege lakini wachezaji nimeshawaweka vizuri kisaikolojia  kwa kuwaambia kuwa wajue tumekuja vitani.

 

"Tulipata shida sana jana kwani mpaka saa nne usiku wachezaji walikuwa hawajapata chakula na ilibidi wale mikate tu  lakini leo tumeweka  utaratibu wa kupata chakula kizuri ili tuingie uwanjani tukiwa na lengo la ushindi," alisema Nkoma.

 

Naye nahodha wa Tanzanite, Wema Richard alisema wamejipanga vizuri kupambana na kupata ushindi huku akiwataka Watanzania kuwaombea kwani mchezo huo ni mgumu kwa sababu wako ugenini lakini watajitahidi kwa uwezo wao kuhakikisha wanarudi na ushindi nyumbani.