Tanzanite Stars yakabidhiwa bendera

Muktasari:

Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo, Yusuph Singo aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanafuzu Kombe la Dunia kwa manufaa yao na nchi.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Wanawake wenye umri wa miaka  20 'Tanzanite Stars' leo imekabidhiwa bendera kabla ya safari ya kuelekea Nigeria kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Ufaransa, 2019.
Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo, Yusuph Singo aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanafuzu Kombe la Dunia kwa manufaa yao na nchi.
"Wachezaji, mnapokwenda kule mnatakiwa mfahamu kuwa mna jukumu la kuipeperusha bendera tukufu ya Tanzania na kutuwakilisha Watanzania zaidi ya milioni 50. Lakini pia hii inaweza kuwa fursa kwenu kujitangaza kimataifa kama mnavyoona siku hizi wachezaji wa Tanzania wameanza kuchukuliwa kwa wingi kwenda nje," alisema Singu.
Kocha wa Tanzanite, Sebastian Mkoma alitamba kuiduwaza Nigeria kwa kuitupa nje ya mashindano hayo.
"Tumejiandaa vizuri ingawa tulikosa mechi za kirafiki za kimataifa, tutahakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Mkoma