Tanzania yazisindikiza timu za Kenya, Uganda

Muktasari:

Mpambano mwingine ulikuwa kati ya Wanaume Kenya dhidi ya Tanzania ambao ni wenyeji na kushuhudia Wabongo wakilala kwa pointi 9-8.

Mwanza. Timu za Kenya (Wanaume) na Uganda (Wanawake) zimeanza vyema mashindano ya Baseball na Soft Ball, huku Tanzania ambao ni wenyeji wakiambulia patupu kwenye mechi za ufunguzi.

Michuano hiyo ya Afrika Mashariki ambayo yamezinduliwa leo Ijumaa jijini Mwanza kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mazoezi iliyoko Butimba, imeshuhudiwa timu ya Wanawake ya Uganda na ya Wanaume kutoka Kenya zikitakata kwa kuzitembezea vichapo timu pinzani.

Mechi ya kwanza, Uganda ilikipiga na Kenya kwenye mchezo wa Soft Ball (Wanawake) na Kenya kuangukia pua kwa kukubali kulala kwa pointi 14-3.

Kutokana na matokeo hayo makocha wa Kenya na Uganda kila mmoja alijinasibu kuibuka bingwa kwenye michuano hiyo.

Kocha wa Uganda, Otim Allan alisema kuwa wao wamekuja kwa nia ya kutwaa ubingwa na kuweka historia.

"Tumekuja kushindana na ushindi huu unatupa nguvu zaidi kutamba kwamba lazima malengo yetu yatimie," alisema Allan.

Kwa upande wake Kocha wa Kenya, Mukiibi Meddle alisema kuwa licha ya kuwahofia Uganda kumtibulia mipango yake, lakini anamini kikosi chake kitakuwa bingwa.

"Naona Uganda ndio timu nzuri na ngumu kwenye mashindano haya, lakini kwa ujumla timu zangu ziko vizuri zaidi na matarajio yangu ni ubingwa," alisema Meddle.

Mashindano hayo yanatarajia kumalizika Jumapili, ambapo kila timu inachuana kutwaa ubingwa.