Waogeleaji Tanzania wakusanya medali 9 za dhahabu

Muktasari:

  • Siku ya kwanza Tanzania ilifanikiwa kutwaa jumla ya medali 21 zikiwamo tisa za shaba.

WAOGELEAJI wa Tanzania wameendelea kung’ara katika mashindano ya Cana ya Kanda ya tatu ya Afrika baada ya kukusanya medali mbalimbali kwa siku ya pili mfululizo.

Kutokana na kutawala mashindano hayo, matumaini ya timu hiyo ya Taifa kulitetea taji hilo yameongezeka na wanatarajia kuweka historia ya pili kwa kutwaa ubingwa wa jumla wa mashindano hayo.

Siku ya kwanza, Tanzania ilitwaa medali zaidi ya 21, huku ikishinda  tisa za dhahabu, tano za shaba na saba za fedha katika mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Sudan na wenyeji Tanzania.

Muogeleaji wa kwanza wa Tanzania kutwaa medali ya  dhahabu ni Natalie Sanford ambaye alishinda mita 800 kwa staili ya freestyle kwa waogeaji waliochini ya miaka 14 na baadaye muogeleaji nyota wa Tanzania wa kike, Sonia Tumiotto akishinda kwa waogeleaji wa kike wenye umri zaidi ya miaka 15.

 Waogeleaji wengine waliotamba na kutwaa medali za dhahabu ni, Elia Imhoff, Natalie, Emma Imhoff, Tara Behnsen, Marin De Villard na kwenye ‘relay’ kupitia kwa Sonia Tumitto, Collins Saliboko, Hilal Hilal na Emma Imhoff.

Kocha wa timu hiyo, Michael Livingstone alisema kuwa wana matumaini makubwa ya kutetea ubingwa huo pamoja na upinzani mkali kutoka kwa nchi shiriki hasa Zambia.

“Mashindano ni magumu sana, ushindani ni mkubwa, tuna uhakika asilimia 100 kuwa tutashinda, waogeleaji wetu wamefanya vyema katika mashindano ya awali na tunaongoza kwa kutwaa medali,” alisema Michael.

Alisema kuwa wamefuraishwa sana na jinsi waogeleaji wao wanavyojituma kwa kutambua kuwa wapo nyumbani nna kukataa kata kata kushindwa.

Mashindano hayo yaliyoanza Alhamisi, yatafungwa leo saa 11.00 jioni na ambapo zawadi mbalimbali za washindi zitatolewa.