Kili Stars yanyukwa, Z'bar yatupwa kwa Uganda

Muktasari:

Zanzibar Heroes ndio ilikuwa ya kwanza kuonja kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Libya, shukrani kwa goli la Alharaish Zakaria alilolifunga dakika ya 24.

Nairobi.Timu zote za Tanzania zimeambulia kipigo cha bao 1-0, katika michezo yao ya leo Jumatatu ya kukamilisha ratiba dhidi ya Libya na Kenya kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.
Zanzibar Heroes ndio ilikuwa ya kwanza kuonja kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Libya, shukrani kwa goli la Alharaish Zakaria alilolifunga dakika ya 24.
Mchezo wa pili Kilimanjaro Stars iliaga kwa aibu mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kenya lililofungwa na Vincent Ouma katika dakika 19.
Kutokana na matokeo hayo,Kilimanjaro Stars inarejea nyumbani ikiwa na pointi moja baada ya kupoteza michezo mitatu na kutoa sare mchezo mmoja.
 Wakati Kili Stars ikiondoka na aibu hiyo ndugu zao wa Zanzibar Heroes ina kibarua kikubwa cha kupambana na Uganda katika nusu fainali ya mashindano ya Chalenji itakayofanyika Ijumaa.
Nusu fainali nyingine itazikutanisha wenyeji Kenya na Burundi katika mchezo utakaofanyika Alhamis.
Zanzibar Heroes imemaliza nafasi ya pili kwenye kundi A ikiwa na pointi sana huku Kenya ikiongoza kundi hilo ikiwa na pointi nane,nafasi ya tatu imeshikwa na Libya yenye pointi sita,Rwanda ni ya nne kwa kuwa na pointi nne wakati Kili Stars imeshika mkia kwa kuwa na pointi moja.
Katika kundi B,Uganda wamemaliza vinara kwa pointi tano sawa na Burundi wakifuatiwa na Ethiopia iliyovuna pointi nne na Sudan Kusini ikishika mkia kwa kukusanya pointi moja.