Taita amvulia kofia Maxime

Muktasari:

Kagera Sugar msimu huu iliweka rekodi ya kucheza mechi saba za mwanzo wa ligi bila ya kushinda

Dar es Salaam. Beki wa kulia wa Kagera Sugar, Godfrey Taita ameshindwa kuvumilia na kutamka, kocha wake Mecky Maxime ni mpambanaji kama angekuwa mwingine kwa namna timu yao ilivyokuwa na matokeo mabaya angekuwa ameshaachia ngazi mapema.

Taita alisema, Maxime hakujali aina ya matokeo waliyokuwa wanayapa hapo awali, lakini akawa anatafuta mbinu mbalimbali kuhakikisha timu inashinda na inakaa katika nafasi nzuri.

Beki huyo wa zamani wa Yanga, amebainisha mbinu aliyokuwa anaitumia Maxime ni kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia na kuwaongezea morali wa kupambana bila kukata tamaa.

"Kweli nimeamini Maxime ni mpambanaji, kwa hali ilivyokuwa siku nyingine angekuwa ameikimbia aibu, lakini ni kama daktari ambaye hupambana hadi mwisho kuhakikisha anamnusuru mgonjwa hata katika mazingira magumu ya aina gani."

Kagera ipo nafasi ya 11 kati ya timu 16 kwenye Ligi Kuu ikiwa na pointi 22, lakini hali ilikuwa mbaya zaidi mwanzoni mwa msimu, ilikuwa ikipishana nafasi tatu za mkiani na ilishang'olewa katika michuano ya Kombe la FA na Buseresere ya Geita.